Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 22,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (Shirika la Viwango Tanzania (TBS)) imeendelea kuimarisha mifumo ya ubora wa bidhaa nchini kwa kuhakikisha viwango mbalimbali muhimu vinakamilishwa na kutumika katika sekta za kilimo, chakula na uhandisi.
Amesema hadi kufikia Aprili, 2026 jumla ya viwango 230 vilikuwa vimekamilika, huku viwango vingine 499 vikiwa katika hatua za mwisho za maandalizi na vinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027,bungeni Waziri Kapinga amesema jumla ya leseni 856 za nembo ya ubora ya TBS zilitolewa, sawa na asilimia 85.6 ya lengo la kutoa leseni 1,000 kwa mwaka.
Kati ya leseni hizo, 349 zilitolewa kwa wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama vile siagi ya karanga, asali, maji ya kunywa, mchele na bidhaa nyingine.
Vilevile, amesema Shirika hilo limeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wadau mbalimbali kuhusu kuzingatia mifumo ya ubora ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyohitajika.
Pia amesema hadi kufikia Aprili, 2026 jumla ya bidhaa 2,070 za chakula na vipodozi zilikuwa zimesajiliwa, sawa na asilimia 86.3 ya lengo la kusajili na kutoa vibali 2,400 kwa mwaka.
Amesema bidhaa hizo 1,406 ni za chakula na 664 ni za vipodozi, hatua inayolenga kulinda afya za watumiaji na kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.