Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 22,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji kupitia maboresho ya miundombinu katika Kongani ya Viwanda ya TAMCO Industrial Area iliyopo wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, hatua inayolenga kuongeza tija ya viwanda na kuvutia wawekezaji wapya.
Kongani hiyo ambayo ni moja ya maeneo muhimu ya viwanda nchini inatumika kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo uunganishaji wa mitambo na magari, uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, bidhaa za viwandani pamoja na huduma saidizi.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027,bungeni Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga,amesema kuwa eneo hilo lina jumla ya viwanda 14, ambapo viwanda 12 tayari vinafanya kazi huku viwili vikiwa katika hatua za mwisho za uwekezaji.
“Hadi kufikia Aprili 2026, Serikali imefanikiwa kuboresha miundombinu muhimu ndani ya kongani hiyo, ikiwemo ujenzi wa kilomita 1.8 za barabara za ndani kwa kiwango cha lami, hatua iliyosaidia kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na vifaa ndani ya eneo hilo la viwanda.”amesema Mhe.Kapinga
Aidha, miundombinu ya umeme imeimarishwa, hali iliyowezesha wawekezaji kupata umeme wa uhakika, jambo linalochochea ufanisi wa uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji wa viwanda.
Viwanda vinavyofanya kazi katika kongani hiyo ni pamoja na Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), Hester Bioscience Ltd, Global Packaging (T) Ltd, Motor Hub East Africa Ltd (TATA Holdings), China Boda Ltd, New Force Company Ltd, Konfa Enterprises, Loti Energies, Hero Sound Traders Ltd, UC General Investment Limited, GF Assemblers Ltd na Fortes Energies Ltd.
Amesema viwanda hivyo vimefanikiwa kuzalisha ajira 853, hatua inayotoa mchango muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi wa maeneo ya jirani.
Serikali imeeleza kuwa maboresho yanayoendelea yameanza kuvutia wawekezaji wapya, wakiwemo Hyundai Motor Company ambao wanaandaa kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari nchini.
Pia, kampuni ya Goodlife Investment Tanzania inatarajiwa kuanza uunganishaji wa magari ya umeme (Electric Vehicles), huku Sanda Max Group Limited ikiendelea na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo.
Serikali imesisitiza kuwa uwekezaji huo mpya utaongeza mnyororo wa thamani wa viwanda, kukuza ajira zaidi, kuongeza mapato ya ndani na kupunguza gharama za bidhaa zinazotumika nchini.
Aidha amesema maboresho ya miundombinu katika TAMCO yanatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi ya viwanda nchini, yakilenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.