Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo bnlog-DODOMA
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetaja vipaumbele vitano vya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/27 vinavyolenga kuimarisha ubora wa elimu, kuongeza ujuzi kwa vijana pamoja na kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia nchini.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itaendelea kutekeleza sera na mitaala ya elimu, kufanya mapitio ya sheria pamoja na kuandaa miongozo na kutoa mafunzo mbalimbali nchini.
Aidha amesema Serikali itaongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali ili kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajiriwa kwa kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
Profesa Mkenda amesema kipaumbele kingine ni kuongeza fursa na ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu sambamba na kuimarisha elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na ushindani wa kimataifa.
Pia amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya Taifa.