Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali imebadili mtazamo katika kusimamia sekta ya viwanda na biashara kwa kuweka mkazo kwenye uwezeshaji badala ya udhibiti, akisisitiza kuwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo hazitakuwa “polisi wa biashara” bali washirika wa biashara katika kukuza uchumi wa taifa.
Akichangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma Juni 22, 2026, Mhe. Kapinga amesema sekta ya viwanda na biashara ndiyo nguzo muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira kwa vijana, kuongeza pato la taifa, kuharakisha matumizi ya teknolojia na kuimarisha biashara ya kimataifa.
Amesema wabunge wamejadili kwa kina umuhimu wa kuanzisha viwanda vipya vya kimkakati, kuvilinda viwanda vilivyopo, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mazingira ya biashara, huku Serikali ikiahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.
Mhe. Kapinga amesema Bajeti ya mwaka 2026/2027 imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia punguzo la kodi kwa viwanda vipya, unafuu wa kodi kwenye mitambo na vifaa vya uzalishaji, pamoja na kupunguza ushuru kwa malighafi zinazotumika viwandani.
Ameeleza kuwa taasisi 13 zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, zikiwemo TBS na BRELA, zina jukumu la kufungua fursa za biashara na siyo kuwa kikwazo cha ukuaji wa sekta hiyo “Sisi siyo mgambo wala polisi wa biashara, Tunataka kuwa marafiki wa wafanyabiashara, kuwaelekeza, kuwawezesha na kujenga mazingira bora ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
