Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amehimiza wananchi hususan vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana kutokana na uhifadhi wa mazingira ili kujipatia kipato.
Dkt. Muyungi ametoa msisitizo huo alipofanya ziara katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila kilichopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma leo Julai 15, 2026.
Alisema katika ziara hiyo amejionea namna mradi huo unavyoweza kuchagiza sekta ya uchumi wa buluu ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia kwa kuhamsisha ufugaji wa samaki ambao huchangia kipato.
Aidha, Dkt. Muuyungi alieleza kuwa hifadhi endelevu ya mazingira ambayo imechangia kuwepo kwa mabwawa ya kuzalisha na kufugia samaki katika eneo hilo imegeuka fursa.
“Vijana wachangamkie fursa hizi za usimamizi wa taka kwani hapa katika kituo hiki tumeona namna taka hizo zinavyogeuzwa kuwa chakula cha samaki hivyo tusafishe mazingira yetu tukusanye taka na tuzigeuze fursa, tutapata kipato,” alisema.
Sanjari na hilo Dkt. Muyungi aliongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Maamu wa Rais katika utekelezaji wa Dira 2050 ambayo nguzo ya tatu inazungumzia masuala ya hifadhi ya mazingira, ni hatua mojawapo ya kuhakikisha Sera ya Uchumi wa Buluu inatekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila Bw. Lucka Mgwena alisema kituo hicho ambacho kinasimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaendelea kuibua teknolojia rafiki kwa mazingira hasa kwa wafugaji wa samaki.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchagiza sekta ya uchumi wa buluu ambayo imeendelea kukua kwa kasi na kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Bw. Mgwena alisema kupitia mradi huo wafugaji wa samaki wanaweza kupata mbegu (vifaranga) za samaki ambazo zinazalishwa kwa njia ya kitalaamu na hivyo kuongeza tija katika sekya hiyo.
“Katika Mkoa wa Ruvuma kuna kilimo cha vyakula na mazao mbalimbali hivyo tumeibua teknolojia ya kuzalisha vyakula vya samaki kwa kutumia taka oza kutokana na mabaki ya vyakula mbalimbali badala ya kuacha taka hizo zikizagaa ovyoo na kuchafua mazingira,” alisema.

