Featured Kitaifa

TOSCI YAFUNGUA FURSA ZA USHIRIKIANO WA MBEGU BORA NA SUDANI KUSINI

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna-DODOMA

Tanzania imeendelea kujijengea heshima katika sekta ya mbegu barani Afrika baada ya Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Sudani Kusini, Mhe. Clement Juma Mbugoniwia, kutembelea banda la Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea Nzuguni, mkoani Dodoma, kujifunza mifumo ya kisasa inayotumika nchini kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Ziara hiyo, iliyofanyika akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ilitoa fursa kwa ujumbe huo kupata maelezo ya kina kuhusu hatua zinazochukuliwa na TOSCI katika kusimamia ubora wa mbegu kuanzia uzalishaji, uhakiki hadi usambazaji wake kwa wakulima, mfumo ambao umeendelea kuimarisha imani ya wakulima na wadau wa sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Bw. Nyasebwa Chimagu, alisema taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Sudani Kusini katika kujenga uwezo wa kitaalamu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora wa mbegu ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kukuza biashara ya mbegu bora ndani na nje ya mipaka ya nchi hizo.

Alisema moja ya mafanikio makubwa ya TOSCI ni matumizi ya mfumo wa kidijitali wa kuhakiki ubora wa mbegu kupitia lebo maalumu za uthibitisho, unaomwezesha mkulima kuthibitisha uhalali wa mbegu kwa kutumia simu ya mkononi kupitia huduma ya *148*52#, baada ya kukwangua lebo yenye namba maalumu.

Mbali na hilo, wakulima wanaweza kupata ushauri na taarifa mbalimbali kupitia namba ya huduma kwa wateja isiyolipiwa 0800 782 424, hatua inayosaidia kupunguza matumizi ya mbegu bandia na kuongeza tija mashambani.

Chimagu alieleza kuwa TOSCI pia inasimamia upatikanaji wa mbegu za awali (Early Generation Seed), ambazo ndizo msingi wa uzalishaji wa mbegu bora, kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na kampuni binafsi za uzalishaji wa mbegu.

Aidha, alisema taasisi hiyo hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ISTA na OECD, vinavyohakikisha mbegu za Tanzania zinakubalika katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Alisema ushirikiano unaoendelea kujengwa kati ya Tanzania na Sudani Kusini katika sekta ya mbegu ni hatua muhimu itakayochochea ubadilishanaji wa teknolojia, maarifa na uzoefu, huku ukifungua fursa za biashara ya mbegu bora na kuimarisha usalama wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

About the author

Alex Sonna