Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Bei za mafuta zinazotumika nchini kuanzia Jumatano, Agosti 5, 2026 zimeshuka kwa shilingi 92 kwa lita ya petroli, shilingi 204 kwa lita ya dizeli na shilingi 440 kwa lita ya mafuta ya taa, hali ambayo itawapa unafuu wa gharama za maisha kwa wananchi, wamiliki wa vyombo vya usafiri, mitambo na viwanda.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Salum Mnuna, inaonesha kuwa, kwa mwezi Agosti 2026, Dar es Salaam petroli itauzwa kwa shilingi 3,898, Tanga shilingi 3,959 na
Mtwara shilingi 3,990. Aidha, dizeli itauzwa shilingi 3978 kwa Dar es Salaam, shilingi 4,039 Tanga na shilingi 4,070 Mtwara. Kwa upande wa mafuta ya taa, kwa Dar es Salaam, Tanga na Mtwara bei itakuwa shilingi 4,003,4,065 na 4,096, mtawalia.
Bw. Mnuna amevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei husika, punguzo, na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika cha mafuta sanjari na kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na EWURA.
“Ni kosa kisheria kutotekeleza maagizo haya na adhabu kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka,” alisisitiza Bw. Mnuna.
Ikumbukwe kuwa, EWURA hutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kila Jumatano ya kwanza ya mwezi ambazo hutumika kwa mwezi husika. Katika miezi ya hivi karibuni, bei za mafuta zimekuwa zikibadilika mara kwa mara kutokana changamoto mbalimbali ikiwemo vita inayoendelea eneo la Mashariki ya Kati.