Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu (wa pili kutoka kushoto) akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Liwale wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoani Lindi, tarehe 4 Agosti, 2026. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mbunge wa Liwale, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde.
Na. OWM ( KAM) – Liwale, Lindi
Serikali imewataka wananchi wa wilaya ya Liwale kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati ikichukua hatua madhubuti kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kilipikwe kata ya Liwale Mjini mkoa wa Lindi leo tarehe 4 Agosti, 2026 ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake Mkoani Lindi.
Waziri Sangu amesema kuwa, amepokea maelezo ya Wazee wa Liwale kuhusu kuwepo kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji hatua inayotishia usalama na kuondoa maelewano baina ya makundi hayo ya jamii.
” Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji. Nimekaa na wazee wa Liwale na nimewaeleza kuwa Serikali hatukubali kuona watu wakiwindana kama wanyama” alisisitiza Waziri Sangu.
Kadhalika, Mhe. Sangu amesema atakwenda kushauriana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Bashir Ally ili kazi ya kutatua migogoro hiyo ifanyike kwa haraka huku jamii ikiendelea kuishi kwa maelewano.
Akiwa wilayani humo, Waziri Sangu alikagua miradi ya ujenzi wa shule mpya ya msingi za Mbaya na RM ambazo kila moja imegharimu milioni 314 ambazo zilizotolewa na Serikali.
Waziri Sangu aliwaeleza wananchi kuhusu mafanikio ya Serikali katika kipindi cha miaka minne ambapo wilaya ya Liwale imepokea Bilioni 3.9 kwa ajili ya huduma za kijamii, Bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za sekondari ambapo pia vijiji 37 ambavyo havikuna na umeme vimeunganishwa na kukamilisha jumla ya vijijini 76 vya wilaya hiyo kuunganishwa na umeme, utekelezaji huwo umefanyika katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha ambaye pia ni Mbunge wa Liwale Mhandisi Mshamu Ali Munde ameshukuru Serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 48 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye miradi ya maemdeleo ikiwemo Sekta ya Afya, Elimu, Maji, Miundombinu pamoja na uwezeshaji wa Wananchi.
Mhandisi Munde aliwaeleza wananchi kuwa ataendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi katika kuhakikisha miradi inatekelezwa ikiwemo barabara ya Nangurukuru hadi Liwale (251 km) inajengwa kwa kiwango cha changarawe na lami kwa kuwa tayari bajeti ya kujenga kwa awamu imetengwa.
Nao wananchi wa Liwale wakizungumzia kero ya Tembo pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji wametaka Serikali kushughulikia haraka suala hilo na kuchukua hatua mapema ili kuimarisha Mahusiano kwa jamii.
Aidha, Waziri Sangu yuko mkoani Lindi kwa ziara ya kiserikali kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali pamoja na kuzungumza na wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka Mawaziri kwenda mikoani kutatua kero na kueleza mafanikio ya Serikali.
