Featured Kitaifa

VIJANA WAHIMIZWA KUINGIA KILIMO BIASHARA KUPITIA MBEGU BORA ZA RIJK ZWAAN

Written by Alex Sonna

 

Na Mwandishi wetu,Dodoma

Kampuni ya Rijk Zwaan Tanzania imetumia Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma kuwahamasisha wakulima na vijana kutumia mbegu bora pamoja na teknolojia za kisasa za uzalishaji wa mboga mboga, ikieleza kuwa hatua hiyo ndiyo njia ya kuongeza tija, kipato na ushindani wa mazao sokoni.

Akizungumza kwenye maonesho ya Nanenane Dodoma Agosti 3,2026, Mtaalamu Mwandamizi wa Maendeleo ya Bidhaa na Afisa wa Kilimo wa Rijk Zwaan Tanzania, Neiman Mollel, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu uzalishaji wa kisasa wa mazao mbalimbali ya bustani kwa kutumia mbegu zenye ubora wa hali ya juu.

Amesema Rijk Zwaan Tanzania kwa sasa inafanya shughuli zake katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Morogoro na Mwanza, ambako imeendelea kuwafikia wakulima kwa mafunzo, ushauri wa kitaalamu na huduma zinazowawezesha kuongeza uzalishaji wenye tija.

Mollel amesema maonesho ya Nanenane ni fursa muhimu kwa wakulima kujifunza mbinu mpya za kilimo cha mboga mboga, hususan mazao ya kabichi, nyanya, hoho, karoti pamoja na mazao mengine yanayohitajika kwa wingi sokoni.

Kwa upande wake, Mhamasishaji wa Kampuni ya Rijk Zwaan Tanzania, Ray Peter Mark, amewataka wakulima na wananchi wanaotembelea maonesho hayo kufika katika banda la kampuni hiyo ili kujifunza kuhusu mbegu bora, teknolojia za uzalishaji na namna ya kupata mavuno yenye ubora na faida kubwa.

Amesema vijana wengi wanaofika kwenye banda hilo huonesha nia ya kuingia katika kilimo cha biashara, lakini changamoto kubwa wanayoitaja ni ukosefu wa mitaji ya kuanzia.

“Tunawaeleza kuwa Serikali imeweka mifuko mbalimbali ya kuwawezesha vijana kupitia Wizara yenye dhamana ya vijana pamoja na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,nawahimiza kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na fursa hizo za kifedha,” amesema.

Amesema pamoja na kusambaza mbegu bora, kampuni hiyo inaendelea kuwashauri wakulima umuhimu wa kuanza kwa kutambua mahitaji ya soko kabla ya kuzalisha, ili kuhakikisha mazao yanayolimwa yanakuwa na uhakika wa wanunuzi na kuwaletea wakulima faida.

Ameongeza kuwa Rijk Zwaan pia inaendelea kuwaunganisha wakulima na masoko mbalimbali, jambo linalowasaidia kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji halisi ya walaji na kuongeza thamani ya mazao yao.

Amesema kupitia elimu hiyo, kampuni inalenga kujenga kizazi cha wakulima wa kisasa wenye uwezo wa kutumia mbegu bora, teknolojia sahihi na taarifa za masoko ili kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika kukuza uchumi wa taifa.

About the author

Alex Sonna