Featured • Kimataifa

TANZANIA, CHINA ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA TVET

Written by Alex Sonna
Na.Mwandishi Wetu,
Wizara ya Elimu Sayansi na Wizara ya Elimu ya China zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kimkakati katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET), kwa lengo la kuongeza ujuzi kwa vijana na kuandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.
Makubaliano hayo yamefikiwa  mjini Tianjin, China, katika kikao cha pamoja kati ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, na Naibu Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Watu wa China Ren Youqun.
Katika kikao hicho  Mhe. Wanu Hafidh Ameir amesema China imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kukuza ma kiend3leza  elimu kupitia ujenzi wa miundombinu, ufadhili wa masomo, mafunzo ya kitaalamu na ubadilishanaji wa wataalamu.
Ameongeza kuwa Miradi kama ujenzi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera imeongeza fursa na ubora wa mazingira ya kujifunzia, kufundishian na kuimarisha elimu nchini.
Ameeleza kuwa Tanzania inalenga kutumia kikamilifu fursa za Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), ikiwemo mpango wa kuanzisha vyuo vinne vya ufundi vinavyolenga kutos mafunzo yanayokidhi mahitaji ya viwanda, teknolojia na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, toleo la 2023, inayosisitiza mafunzo ya vitendo na ujuzi wa kisasa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu wa China, Ren Youqun, amesema Serikali ya China imejipanga kuendeleza mpango wa ufadhili wa wanafunzi na programu za kubadilishana wataalamu na wanafunzi.
Amesema China itaongeza misaada ya kitaaluma na fursa za mafunzo ya ufundi na teknolojia kwa vijana wa Kitanzania ili kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika miradi ya maendeleo.
Ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na China nchini Tanzania imewezesha mafunzo ya vitendo, uboreshaji wa mitaala na ubadilishanaji wa wataalamu kati ya vyuo vya China na Tanzania.
Zaidi ya vijana 2,000 tayari wamenufaika na mafunzo ya ujenzi na uhandisi, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa elimu ya ufundi na kuimarisha msingi wa maendeleo ya kiuchumi nchini.

About the author

Alex Sonna