Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge kuiidhinishia Sh trilioni 2.39 kwa mwaka wa fedha 2026/27 Kwa ajili ya kutekeleza Vipaumbele vitano.
Akiwasilisha Mpango wa mapato na matumizi wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027 leo Mei 7,2026 bungeni,Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda amesema Shilingi bilioni 697.84 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 648.08 ni kwa ajili ya mishahara huku Shilingi bilioni 49.75 zikitengwa kwa matumizi mengineyo.
Aidha, Wizara hiyo imeomba Shilingi trilioni 1.69 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Shilingi trilioni 1.33 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 359.33 zinatarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.