Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DOODMA
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imetangaza vipaumbele vya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/27 vitakavyolenga kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika programu za kimataifa za elimu, sayansi, utamaduni na mawasiliano.
Akiwasilisha Mpango wa mapato na matumizi wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027 leo Mei 7,2026 bungeni,Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda amesema Serikali imechukua juhudi zaidi zitaelekezwa katika kuhakikisha maeneo mbalimbali yenye sifa za urithi na umuhimu wa kipekee nchini yanaingizwa katika orodha ya UNESCO ili kutambuliwa kimataifa.
Kupitia mpango huo, Serikali itakamilisha taratibu za maeneo yaliyopo katika orodha ya awali ya UNESCO pamoja na maeneo mapya yanayotarajiwa kuwasilishwa kwa ajili ya kupata hadhi ya kuwa sehemu ya urithi unaotambuliwa duniani. Hatua hiyo inalenga kuongeza hifadhi ya urithi wa taifa sambamba na kukuza utalii, utamaduni na utambulisho wa Tanzania kimataifa.
Aidha, Serikali imepanga kuimarisha utekelezaji wa programu mbalimbali za UNESCO katika sekta za elimu, sayansi, utamaduni na mawasiliano kwa kuzingatia ajenda ya maendeleo endelevu. Programu hizo zinatarajiwa kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia matumizi ya elimu bora, ubunifu wa kisayansi na uhifadhi wa tamaduni za Taifa.
Katika hatua nyingine, Serikali imeweka mkazo katika kuongeza ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa ya UNESCO ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kulinda na kutetea maslahi ya Taifa katika masuala ya elimu, sayansi na utamaduni.
Mpango huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kutumia fursa zinazotolewa na UNESCO katika kuendeleza maendeleo ya Taifa, kukuza diplomasia ya kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jamii ya kimataifa.