Featured Kitaifa

MHINTE AWATAKA WAFUGAJI KUTOFICHA MIFUGO WAKATI WA UCHANJAJI

Written by mzalendo

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Ndg. Abdul Mhinte amewataka Viongozi Wa vyama vya wafugaji kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazotekeleza zoezi la Chanjo ya Mifugo kuhakikisha wafugaji hawafichi mifugo wakati wa uchanjaji ili kufanikisha lengo la serikali la kutokomeza magonjwa kupitia chanjo zinazozalishwa nchini.

Naibu Katibu Mkuu Ndg. Mhinte amesema hayo leo Desemba 19, 2024 wakati akifunga kikao kazi cha Uhamasishaji wa Kampeni ya Chanjo Kitaifa ambayo imefanyika kwa siku mbili katika Ukumbi Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuwataka wafugaji kutii Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya Mwaka 2003 na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji za Mwaka 2020.

“Unakuta mfugaji ana ng’ombe 500 halafu anachanja 100 wengine anawaficha porini baadaye zoezi letu linaonekana lina shida, niwaombe viongozi wa Vyama vya Wafugaji na wafugaji tushirikiane, msifiche mifugo wakati wa uchanjaji” asemema Mhinte.

Aidha, amewahimiza wafugaji kuendeleza maeneo ya malisho ya mifugo itakayosaidia kuondoa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo Dkt. Benezeth Lutege amesema chanjo ya mifugo inayoenda kutolewa awamu hii inazalishwa na Serikali ya Tanzania na imethibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), hivyo wafugaji wathamini chanjo zinazozalishwa nchini.

“Kampeni yetu itatumia chanjo inayozalishwa na Viwanda vyetu vya ndani, ni chanjo salama na imethibitishwa na TMDA pia imepata kibali cha maabara ya Kanda ya Afrika na tumekuwa tukisafirisha hata nje ya nchi” alisema Dkt. Lutege.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho Gabriel Bura amesema zoezi la Chanjo ya Mifugo liende sambamba na uzalishaji wa malisho ili mifugo inapochanjwa iwe imepata chakula kuwezesha chanjo hiyo kufanya kazi .

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ufugaji Tija (CHAMAUTA) Ester Moreto amesema bado elimu inahitajika kuongeza Uelewa kwa wafugaji ili kutokomeza Magonjwa ya Mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo yanayozalishwa nchini.

“Mimi nina miaka minne ninachanja ng’ombe wangu na hawajawahi kuwa na shida yeyote niwaombe wafugaji wenzangu wasifiche mifugo wachanje wote, pia serikali itoe elimu na hamasa kwa wafugaji kote nchini” Alisema Ndg. Moreto.

Mkutano huo wa siku mbili uliotangliwa na Uzinduzi wa Uhamisishaji wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa umefanyika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ambapo Wataalam wa Sekta ya Mifugo, wafugaji na wadau wa afya na mazingira wamesisitiza ushirikishwaji wa wafugaji kwa kuwapa elimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi la chanjo itakayoanza kutekelezwa hivi karibuni.

About the author

mzalendo