Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe Dkt Festo Dugange amewataka waganga wafawidhi kuimarisha ushirikiano wao na watumishi wanao waongoza ili kuleta ubora wa huduma katika kuwahudumia wananchi.
Dkt. Ndugange ameyabainisha hayo leo Februari 13,2024 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi nchini.
Aidha amesema kuwa serikali haitomvumilia mtoa huduma yeyote ambaye atashindwa kusimamia usalama wa vifaa tiba vinavyopelekwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Ni Jukumu lenu Waganga wafawidhi kuhakikisha mnasimamia kwa ufanisi mkubwa vifaa tiba na kuvitumia kwa matumizi sahihi na si vinginevyo” amesema Dkt. Dugange.
Hata hivyo amesema kuwa anataka kutenga bajeti katika kila mwaka wa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu Halmashauri 47 zilitenga fedha kwaajili ya mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albino) hivyo ni vyema katika utoaji wa huduma kuwatambua ili wapate mafuta hayo yatakayowakinga na vitu mbalimbali.
“Tuzingatie utoaji wa huduma kwa watu wenye mahitaji maalum hasa Albino, tengeni bajeti ya mahitaji maalum kulingana na mahitai yao, utengaji wa fedha kwaajili ya mafuta maalumu kwa wenye ualibino ni maelekezo ya serikali na ni ya muhimu” amesema Dkt. Dugange.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewataka waganga hao kupita katika maeneo yanayotoa huduma kuangalia wananchi wanavyopata huduma ikiwemo kuangalia muda wanaokaa na kusubiri kupata huduma badala ya kukaa ofisini.
“Nasisitiza daktari, muuguzi, mtaalamu wa maabara na wengine wote piteni mawodini na kufungua majalada ya wagonjwa kuona huduma gani wagonjwa wamepatiwa tangu wamefika hospitali, je wanapata dawa na vipimo vilivyoandikwa, watumishi wapo na kama wanawajibika”. Amesisitiza Dkt. Magembe.
Sambamba na hayo amewataka watumishi hao wasijifungie maofisini bali watumie ujuzi wao kama viongozi wa vituo kuhakikisha wanatoa Huduma bora kwa wananchi ili kuleta thamani ya uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Waganga wafawidhi wa vituo vya huduma za afya Msingi Tanzania bara you Dkt. Florence Hilari ,amesema kuwa watazingatia maelekezo waliyopewa na kuyafanyia kazi kwa ufanisi na hatimaye kutoa Huduma bora.