Featured Kitaifa

AJALI:BASI LA SHULE LAUA  WATU 10,WANAFUNZI 8,RAIS SAMIA AWALILIA ATUMA SALAMU ZA POLE

Written by mzalendoeditor

Mashuhuda wakilitazama basi la Shule ya King David likiwa limetumbukia mtaroni katika eneo la Mikindani, Mtwara

Basi la Shule ya King David likiwa limetumbukia mtaroni katika eneo la Mikindani, Mtwara

Basi la Shule ya King David likiwa limetumbukia mtaroni katika eneo la Mikindani, Mtwara.

…………………………

 Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kufuatia basi la wanafunzi wa Shule ya King David Mtwara lenye namba za usajili T 207 CTS lililopata ajali asubuhi ya leo Jumanne, Julai 26, 2022 eneo la Mikindani Mtwara likiwa na wanafunzi na kuua watu 10 wakiwemo wanafunzi nane wa shule hiyo.

RAIS SAMIA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Brigedia Jenerali Marco Gaguti kufuatia vifo vya watu 10 vilivyotokea katika ajali ya gari.

Ajali hiyo imetokea leo saa moja asubuhi katika eneo la mteremko la Mjimwema, Kata ya Magengeni, kuelekea Mitengo, Mikindani, Mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Nicodemus Simon Katembo, waliopoteza maisha ni watoto 8 (wasichana 5 na wavulana 3) na watu wazima 2 ambao ni dereva na msaidizi wa gari hilo. 

Majeruhi ni 19 (wasichana 13 na wanaume 6) ambao wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

ACP Katembo amesema ajali hiyo imehusisha basi dogo la wanafunzi aina ya Hiace lenye namba ya usajili T 207 CTS mali ya shule binafsi ya awali na msingi ya King David iliyopo mkoani humo.

Ajali hiyo imetokana na gari hilo kushindwa kuhimili breki katika mteremko na kupoteza mwelekeo na hivyo kutumbukia kwenye korongo. 

Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. 

Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina.

About the author

mzalendoeditor