Featured Kitaifa

KAMBI YA SKAUTI YA KIMATAIFA KUJENGWA CHIGONGWE DODOMA

Written by mzalendoeditor

Na WyEST,MWANZA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepata eneo la ujenzi wa kambi ya Skauti yenye hadhi ya Kimataifa katika eneo la Chigongwe Jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa Jijini Mwanza Februari 19, 2022 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) alipomuwakilisha rais wa Skauti ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (Mb) katika maadhimisho ya Siku ya Mwanzilishi wa Skauti Duniani, Sir Baden Powel.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imewezesha utoaji wa mafunzo kwa walimu walezi wa Skauti wapatao 300 wa shule za Msingi na Sekondari.

“Niwahakikishie kuwa Wizara itaendelea kutoa mafunzo haya kwa walimu ambao bado hawajayapata,” amefafanua Mhe. Kipanga.

Aidha, Mhe. Kipanga ametoa rai kwa viongozi wote wa Chama cha Skauti Tanzania ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kuthamini dhamana kubwa waliyopewa ya malezi ya vijana wa Kitanzania na kuwaasa kuyaishi maneno yaliyotamkwa na mdhamini wa chama hicho mwaka 2018, Alhaji Ali Hassan Mwinyi yenye ujumbe wa ‘maisha yetu ni hadithi.’

“Ningependa kila skauti ayaishi maneno haya ili kuepuka tabia za aibu zenye kudhalilisha utu wa mtu tukiwa tumebeba sura ya wengi tunaowawakilisha,” amesema Naibu Waziri Kipanga.

Mhe. Kipanga amewapongeza Skauti hao kwa kuadhimisha siku hiyo kwa kuacha alama kwenye jamii na Taifa kwa ujumla na kawahimiza kuendelea kuziishi kanuni na kiapo cha Skauti kwani ndizo zinazowatofautisha wao Taasisi nyingine.

About the author

mzalendoeditor