Na MwandishiWetu, Dodoma
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma, Profesa Razack Lokina amesema chuo hicho kupitia wataalamu wao na wataalamu wabobezi wataendelea kutoa huduma za afya kwa watanzania ili kuhakikisha jamii inaelimishwa ipasavyo na kuweza kuzuia magonjwa pamoja na kugundua mapema ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati muafaka.
Prof. Lokina ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akihitimisha Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Shule ya Sayansi ya Afya (USCHe),
lililofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 11 hadi 13 Juni 2025 katika Ukumbi wa Jiji, Mji wa Magufuli, mkoani Dodoma.
“Chuo kikuu cha Dodoma kitaendelea kuandaa makongamano mengine yatakayofuata baada ya hili ikiwa ni sehemu ya mipango endelevu ya kuwa na jukwaa la la kudumu kila mwaka la UDOM la kisayansi la afya,”amesema.
Aidha, amebainisha kuwa kongamano hilo lilitoa fursa kwa washiriki kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bunifu za kisayansi katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazokumba jamii.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Dkt. Alfred Meremo, amewashukuru washiriki, wadhamini na wadau wote walioshiriki na kuchangia kufanikisha kongamano hilo. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika tafiti na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya afya ya jamii.
Pia, Dkt. Meremo ameeleza kuwa hadi kufikia hitimisho la kongamano hilo, UDOM ilikuwa imefanya shughuli mbalimbali ikiwemo mbio zisizokuwa na ushindani pamoja na kutoa huduma za kijamii kupitia kambi maalumu iliyohusisha utoaji wa elimu, uchunguzi wa awali na matibabu kwa wakazi zaidi ya 600 katika Hospitali ya Hombolo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Kessy Charles Shija, amesema wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na UDOM kupitia ushirikiano kati ya taasisi hizo, hususan katika kuongeza nguvu kazi kupitia wanafunzi wa fani za uuguzi na udaktari.
“Tumeshirikiana katika uanzishwaji wa huduma muhimu sana za ubingwa wa juu ikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uroto na pia tupo kwenye mchakato wa kuanzisha kituo kikubwa cha matibabu ya saratani. Tunashukuru sana kwa mchango mkubwa wa Chuo Kikuu cha Dodoma,” ameeleza Profesa Shija.
Naye Dkt. Pius Kagoma, akiwasilisha salamu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, amesema kutokana na ofisi hiyo kuwa na jukumu la kusimamia afya katika ngazi ya msingi, ni muhimu kwa wahudumu wa afya kutoka kila halmashauri kushiriki kikamilifu katika kongamano lijalo ili kunufaika na maarifa yatokanayo na tafiti za wataalamu kutoka UDOM.
“Tutatumia kongamano lijalo kuona namna gani hawa wahudumu wa afya ngazi ya msingi wanashiriki na kupata maarifa, na ikiwezekana wawe sehemu ya kamati ya maandalizi ili wapate uzoefu wa kutosha na kusaidia kuboresha huduma kwa jamii,” amesema Dkt. Kagoma.
Washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wataalamu wa afya, watafiti, wanafunzi, na wadau wa sekta ya afya, wamekutana katika Kongamano hilo.
Mada kuu ya kongamano hilo ilikuwa: “Kujadili Mazoea yanayotokana na Ushaidi wa Utafiti na Uvumbuzi katika Kushughulikia Changamoto za Kiafya.” Katika kipindi hicho, jumla ya tafiti mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa lengo la kuchochea matumizi ya ushahidi wa kitaalamu katika maamuzi ya kisera na kiutendaji kwenye sekta ya afya.