Featured • Kitaifa

AIRTEL AFRICA YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA KUPITIA UBUNIFU, UWEKEZAJI NA USHIRIKIANO

Written by Alex Sonna

 

 Kampuni ya Airtel Africa imesisitiza tena dhamira yake ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake milioni 183.5 barani Afrika. Hatua hii itafikiwa kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu ya mtandao, teknolojia za kisasa, na ushirikiano wa kimkakati. Malengo makuu ni kupanua wigo wa huduma na kuongeza uwezo wa mtandao ili kuchochea ujumuishaji wa kidijitali na kifedha kote barani Afrika.

Akizungumza mwanzoni mwa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema:

“Kaulimbiu ya mwaka huu, ‘The Extra Mile’ (Kwenda Hatua ya Ziada), inaendana na dhamira yetu ya dhati ya kuwathamini wateja wetu. Tunafanya hivyo kwa kuboresha jinsi tunavyowahudumia, kusikiliza na kujifunza kutoka kwao, na kuchukua hatua madhubuti zinazolingana na mahitaji na matarajio yao.”

Bw. Taldar pia aligusia uzinduzi wa hivi karibuni wa kibiashara wa huduma ya Airtel ya satelaiti ya moja kwa moja hadi kwenye kifaa (direct-to-device), inayolenga kuziunganisha jamii za vijijini ambazo hazijafikiwa na mtandao au zinazopata huduma duni. Huduma hii inawawezesha wateja wa Airtel wenye simu janja zinazokubaliana na mfumo huo kuendelea kuwasiliana hata katika maeneo yasiyofikiwa kabisa na minara ya kawaida ya ardhini.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Airtel Africa imeongeza zaidi ya minara (tovuti) mipya 3,250 na kilomita 3,200 za mkongo wa mawasiliano (fibre). Aidha, kampuni hiyo inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika maduka yake na njia nyingine za usambazaji, huku ikitumia Akili Bandia (AI) kuboresha zaidi huduma za kidijitali kwa wateja wake

Ili kuwalinda wateja dhidi ya jumbe za matangazo yasiyotakiwa na za utapeli, kampuni ya Airtel imezindua huduma ya Spam Alert (“Kataa Matapeli”). Huduma hii ya bure inatumia mfumo wa Akili Bandia (AI) kutambua na kutoa taarifa za SMS zinazotiliwa shaka mara moja.

Kuthibitisha nia yetu ya kutoa huduma bora, timu ya Airtel itatembelea masoko 14 nchini ili kukutana na wateja, kusikiliza maoni yao, na kubuni mbinu mpya zitakazoongeza ubora na uaminifu wa huduma zetu.

About the author

Alex Sonna