Featured Kitaifa

SERIKALI KUIMARISHA ULINZI WA MITANDAO NA MIUNDOMBINU YA TEHAMA 2026/27

Written by Alex Sonna

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah  Kairuki,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 30,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali imepanga kuongeza nguvu katika kulinda usalama wa mitandao na kuboresha miundombinu ya TEHAMA katika Mwaka wa Fedha 2026/27, hatua inayolenga kuendana na kasi ya matumizi ya teknolojia nchini.

Hayo yamesemwa leo Aprili 30 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah  Kairuki wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri  Kairuki amesema kuwa  serikali imejipanga kuhakikisha mifumo ya kidijitali inalindwa dhidi ya vitisho vya mtandaoni vinavyoendelea kuongezeka duniani.

“Katika juhudi hizo, wizara itatoa mafunzo ya usalama wa mtandao kwa watumishi 80 wa serikali na 20 kutoka sekta binafsi, huku pia ikitoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia.”amesema Mhe.Kairuki

Hatua nyingine muhimu ni kuhuisha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na changamoto mpya za kiusalama. Aidha, serikali itaandaa mpango maalum wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa usalama wa mtandao.

Katika kuimarisha uratibu, wizara itaanzisha Kamati ya Kitaifa ya Usalama wa Mtandao pamoja na kusimamia utendaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ili kuhakikisha taarifa za wananchi zinalindwa ipasavyo.

Sambamba na hilo, juhudi za kuboresha miundombinu ya TEHAMA zitaongezwa, ikiwa ni pamoja na kuendeleza Mkakati wa Kitaifa wa Brodibendi na Mpango Kabambe wa Miundombinu ya TEHAMA. Serikali pia itafanya maboresho ya Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data kilichopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Katika hatua ya kuimarisha huduma za taasisi za umma, serikali itasambaza miundombinu ya mkongo wa mwisho (Last Mile Optic Fiber) kwa taasisi 100 za haki jinai na ulinzi na usalama, zikiwemo mahakama, polisi na magereza.

Aidha, vifaa vya kisasa vya mikutano ya video vitawekwa na kuboreshwa katika wilaya 100 nchini, hatua itakayorahisisha mawasiliano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za serikali.

Mpango huo unaonyesha dhamira ya serikali ya kujenga mfumo imara wa kidijitali unaolinda taarifa, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuweka mazingira salama kwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

About the author

Alex Sonna