Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongoro Jijini Mwanza ikiwa imesalia siku moja maonesho hayo kutamatika.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wananchi kuhakikisha wanatumia watoa huduma wenye leseni halali kutoka mamlaka hiyo wakati wa kununua bidhaa za nishati na huduma zinazodhibitiwa, hatua inayolenga kuimarisha usalama na kuwaepusha na hasara zinazoweza kujitokeza.
Ushauri huo umetolewa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la EWURA kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi katika viwanja vya Nyamhongoro, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Musira amesema matumizi ya watoa huduma wasio na leseni yanaweza kuwaweka wananchi katika hatari mbalimbali, ikiwemo kununua mitungi ya gesi ambayo haijafanyiwa uhakiki unaohitajika na hivyo kuwa na uwezekano wa kuvuja, kusababisha mlipuko au kuleta madhara ndani ya nyumba.
Amesema changamoto nyingine ni uwezekano wa wananchi kupata bidhaa zilizo chini ya viwango pamoja na kukosa ulinzi na fidia pale wanapopata majanga kutokana na matumizi ya bidhaa zilizonunuliwa kwa watoa huduma wasio na leseni.
“Kwa mfano, unapoenda kununua mtungi wa gesi kwa mtu asiye na leseni, hata mzani wa kupimia anaweza kuwa hana. Lakini huyu mwenye leseni kutoka EWURA anazijua taratibu zote, hivyo atakuwa na mzani wa kupimia na atakuwa anauza mitungi ambayo imefunikwa vizuri, huku leseni yake ikiwa inaonekana katika eneo lake la biashara,” amesema Musira.
Aidha, Musira amewataka wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa bidhaa za nishati na huduma za maji kuhakikisha wanapata leseni kutoka EWURA na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara hizo ili kulinda usalama wa wananchi na kuepuka kufanya biashara kiholela.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama kwa kuhakikisha kabla ya kununua bidhaa za nishati wanathibitisha kuwa wanapata huduma kutoka kwa mtoa huduma mwenye leseni, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za usalama ili kuzuia majanga yanayoweza kuepukika.