Featured Kitaifa

NM-AIST  KINARA WA MAONESHO YA NANENANE KANDA YA KASKAZINI  2026

Written by Alex Sonna

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imeibuka kinara miongoni mwa Taasisi za Elimu katika Maonesho ya 33 ya Kilimo, Mifugo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika Viwanja vya Themi Njiro, Arusha.

Akizungumzia ushindi huo, Prof. Maulilio Kipanyula, Makamu Mkuu wa NM-AIST, amesema bidhaa bora zinahitaji utafiti na NM-AIST kama Taasisi inayotanguliza ubunifu, imeendelea kubadilisha matokeo ya tafiti kuwa teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto za wakulima na wafugaji.

Amesema teknolojia mbalimbali zinazooneshwa na Taasisi, ikiwemo Mfumo wa Ng’ombe Smart, zinalenga kuongeza tija katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kuwezesha ufuatiliaji wa uzalishaji wa maziwa na taarifa muhimu za mifugo.

Aidha, Prof Kipanyula amesema mwaka huu NM-AIST imekuja na teknolojia zinazolenga kuongeza thamani ya mazao, yakiwemo tumbaku, mazao ya chakula pamoja na vyakula vya mifugo kama kuku na ng’ombe.

Prof. Kipanyula amesisitiza kuwa NM-AIST inaendelea kujipanga kuwa kinara katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika maeneo ya utafiti na maendeleo, sayansi, teknolojia na ubunifu, pamoja na mabadiliko ya kidijitali.

“Ushindi huu ni chachu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi. Mwaka ujao tutakuja na teknolojia mpya kabisa. Mwaka huu tumefanikiwa kuzalisha takribani patent 40, jambo tunalojivunia na linalotupa nguvu ya kuendelea kuzalisha teknolojia na bunifu zenye tija kwa sekta ya kilimo na mifugo.”

About the author

Alex Sonna