Featured • Kitaifa

BoT INAUPIGA MWINGI MASHINDANO YA SHIMMUTA

Written by Alex Sonna
Timu za michezo za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonesha kiwango cha hali ya juu katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA), yanayoendelea mkoani Morogoro.
BoT inashiriki mashindano hayo kupitia timu zake za michezo mbalimbali, zikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa wavu pamoja na riadha.
Katika mchezo wa mpira wa pete, BoT imeanza vyema kwa kuichapa timu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) magoli 20 kwa 18. Aidha, katika mchezo wa pili uliofanyika leo, Novemba 7, 2026, timu ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) iliponea chupuchupu kugaragazwa na BoT baada ya kulazimisha sare ya magoli 23 kwa 23.
Vilevile, timu ya mpira wa miguu ya BoT imepata ushindi mnono wa mabao 4 kwa 1 dhidi ya timu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika mchezo uliofanyika leo Novemba 7 2026. Ushindi huo unaifanya timu ya mpira wa miguu ya BoT kuwa miongoni mwa timu tishio katika mashindano hayo. 
Ushiriki wa BoT katika mashindano ya SHIMMUTA ni kilelezo cha jitahada za Benki Kuu katika kuimarisha afya na kujenga ushirikiano mzuri baina ya watumishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali hatua inayosaidia kustawisha maelewano na kubadilishana uzoefu ili kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ufanisi.
Mashindano hayo yenye kauli mbiu ya ‘Michezo ituunganishe Kuelekea AFCON 2027’ yalianza tarehe 6 Novemba na yanatarajia kuhitimishwa tarehe 21 Novemba 2026.

About the author

Alex Sonna