Featured • Kitaifa

PROF. MBARAWA AMUALIKA WAZIRI WA FEDHA KUTEMBELEA UJENZI WA SGR

Written by Alex Sonna

 

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amemshirikisha Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Lot 4, eneo la Bukene mkoani Tabora, ili kujadili namna ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Profesa Mbarawa amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana na kuwafikia walengwa kwa wakati, wakiwemo wakandarasi wadogo (Sub-contractors), ili kuwezesha kazi kuendelea bila vikwazo.

Amesema Serikali iliwaelekeza wakandarasi wakuu kutafuta wakandarasi wadogo kwa lengo la kuongeza nguvu kazi na kuharakisha utekelezaji wa mradi, ambapo ameeleza kuwa wakandarasi hao wameanza kufanya kazi zinazoonekana licha ya kuingia katika mradi huo kwa muda mfupi.

Ameongeza kuwa kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ndilo linalogharamia kazi zinazofanywa na wakandarasi wadogo, huku Serikali ikitarajia kukutana na kujadiliana namna ya kurejesha fedha hizo bila kuathiri mwendelezo wa utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, amesema suala la fedha si kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kuongeza kasi ya ujenzi.

Amesema Serikali itafuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha hauchelewi na hivyo kuchelewesha maendeleo yanayotarajiwa kuwanufaisha Watanzania.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi kwa wakandarasi na kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa wakati.

Balozi Omari amewapongeza wakandarasi wadogo kwa kazi waliyoifanya ndani ya miezi miwili, akieleza kuwa maendeleo yao yanaonekana na yanatoa matumaini ya kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Profesa Mbarawa amesema Lot 4 ya mradi wa SGR unaoanzia Tabora ina thamani ya dola za Marekani milioni 900, sawa na takribani Sh trilioni tatu.

About the author

Alex Sonna