Featured Kitaifa

SERIKALI YAZIDI KUIMARISHA UTOAJI WA HAKI KUPITIA PROGRAMU YA “SEMA NA WAZIRI”

Written by Alex Sonna
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka kushughulikia malalamiko ya wananchi kupitia programu ya “Sema na Waziri”, ambayo inawapa wananchi fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi wa Serikali.
Akitoa mrejesho wa programu hiyo Aprili 22, 2026 jijini Dodoma, Dkt. Homera amesema imekuwa daraja muhimu kati ya wananchi na serikali katika kutatua migogoro ya kijamii na kisheria.
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake Machi 17, 2026, programu hiyo imepokea jumla ya malalamiko 2,277 ambayo yameanza kufanyiwa kazi, huku wastani wa malalamiko 67 ukipokelewa kwa kila kipindi.
“Programu hii inaendelea kuwa chombo madhubuti cha kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi popote walipo nchini,” amesema.
Akitoa mifano ya baadhi ya kesi zilizopokelewa, Dkt. Homera amesema mwanafunzi Salma Omari wa Chuo cha DIT Kampasi ya Mwanza alikumbwa na changamoto ya mkanganyiko wa kozi uliomfanya kushindwa kuona matokeo yake. Tayari wizara imewasiliana na uongozi wa chuo husika ili kuhakikisha anapata haki yake bila kupoteza muda.
Katika tukio lingine, Joyce Samson kutoka Mvomelo aliripotiwa kukumbwa na tuhuma za utekaji baada ya kumsaidia mtoto aliyepotea, hali iliyosababisha vitisho na unyanyasaji. Wizara imeunda timu ya wataalamu kufuatilia suala hilo na kushirikiana na wataalamu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe ili kuhakikisha haki inapatikana.
Aidha, malalamiko ya fidia ya ardhi kutoka kwa Rahim Mussa Ngema wa Mtwara yameanza kushughulikiwa, ambapo wizara imewasiliana na Wizara ya Ardhi kwa barua ya Aprili 20, 2026 ili kuharakisha utatuzi wa mgogoro huo.
Kwa upande wa ukatili wa kijinsia, wizara imepongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka katika tukio la Simiyu lililohusisha mama aliyekuwa akipigwa na mumewe. Mtuhumiwa amekamatwa na anaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Akizungumzia mwenendo wa malalamiko, Dkt. Homera amesema migogoro ya ardhi inaongoza kwa asilimia 31.3, ikifuatiwa na ajira kwa asilimia 19.4 na madai kwa asilimia 13.4. Masuala mengine ni pamoja na mirathi, msaada wa kisheria na ukatili wa kijinsia. Kwa mujibu wake, asilimia 56.7 ya malalamiko yote tayari yamepatiwa ufumbuzi.
“Tunawahakikishia wananchi kuwa wizara imejipanga kikamilifu kushughulikia malalamiko yote kwa wakati na kwa ufanisi,” amesisitiza Dkt. Homera.
Programu ya Sema na Waziri inaendelea kurushwa mara mbili kwa mwezi, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki na kusikilizwa.

About the author

Alex Sonna