Featured Kitaifa

REA KUWAWEZESHA BABA NA MAMALISHE MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA NISHATI SAFI KOTE NCHINI

Written by Alex Sonna

 

Kundi hilo limeanza kuwezeshwa kupitia Mradi wa majiko banifu ambapo takribani majiko 200,000 ambayo yameanza kusambazwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 kwa njia ya ruzuku ya hadi asilimia 85 ambapo imeelezwa hatua hiyo itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati kwa Watumiaji.

Hayo yameelezwa Aprili 21, 2026 na Mhandisi Mwandamizi kutoka REA, Deusdedit Malulu wakati wa Kongamao la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania lililoandaliwa na Umoja wa Mamalishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Malulu amesema REA imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha Baba na Mama lishe nchini ili watumie teknolojia za nishati safi ya kupikia kupitia Miradi mbalimbali yenye lengo la kupunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo.

“Na inafanya hivyo kwa sababu miongoni mwa majukumu yake ni kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati zote, hususani nishati hiyo safi ya kupikia.”

Amesema ushiriki wa REA katika kongamao hilo umelenga kutoa elimu na kuwafahamisha Washiriki kuhusu fursa zilizopo katika Miradi ya nishati safi, ikiwamo ruzuku ya mitungi ya gesi na majiko banifu.

“Tunayo Miradi mingi inayolenga kuhakikisha Baba lishe na Mama lishe wanapata nishati safi kwa bei nafuu na kwa wingi. Hii ni pamoja na utoaji wa ruzuku kwenye mitungi ya gesi na majiko banifu,” amesema, Mhandisi, Malulu.

Aidha ameongeza kuwa REA imeendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali kuhakikisha teknolojia za nishati safi zinawafikia wananchi katika maeneo yote nchini.

Ameutaja pia Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia hadi kwenye makazi ya Watu; Mradi unaoanzia Mtwara; Lindi hadi Dar es Salaam ambapo hadi sasa kaya takribani 980 zimeunganishwa na mabomba ya gesi asilia ya kupikia kwa ushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mhandisi, Malulu amesema kuwa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi zilianza mwaka 2021; ambapo matumizi yalikuwa kati ya asilimia mbili hadi sita na kwamba hadi sasa matumizi yameongezeka na kufikia takribani asilimia 23 hadi 25.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Amesema kasi ya utekelezaji wa miradi iliyopo inaonesha uwezekano mkubwa wa kufikia lengo hilo mapema.

“Mama lishe na baba lishe ni kundi muhimu sana katika kufanikisha azma hii. Wanapotumia nishati safi wanapunguza gharama na kuboresha mazingira ya kazi zao, hivyo tunawapa kipaumbele katika miradi yetu,” amesisitiza.

Kadhalika, Maluku ameeleza kuwa, REA itaendelea kubuni zaidi Miradi ya kibunifu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa wale wa kipato cha chini, kwa lengo la kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu kwa Wananchi wote.

About the author

Alex Sonna