Featured Kitaifa

EWURA YAONGEZA UFANISI SEKTA YA NISHATI

Written by Alex Sonna

 

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius  Ndejembi, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 22 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha sekta ya nishati nchini inasimamiwa kwa ufanisi kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Hatua hiyo inalenga kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora, salama na zenye uhakika, huku ikiimarisha maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 22,2026 bungeni Dodoma.

Ndejembi amesema kuwa EWURA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Mamlaka hiyo itahakikisha kuwa wadau wote wa sekta ya nishati wanazingatia viwango vinavyotakiwa, kuanzia ujenzi wa miundombinu hadi utoaji wa huduma kwa watumiaji wa mwisho.

“Katika utekelezaji huo, EWURA itaendelea kutoa vibali vya ujenzi wa miundombinu ya nishati pamoja na leseni za biashara kwa waendeshaji mbalimbali wa sekta hiyo. Sambamba na hilo, ukaguzi wa mara kwa mara utafanyika ili kuhakikisha ubora wa miundombinu, pamoja na bidhaa za petroli na gesi asilia unazingatia viwango vilivyowekwa kitaifa na kimataifa.”amesema Mhe.Ndejembi

Aidha, Serikali imeweka mkazo maalum katika kuboresha usimamizi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Kupitia maboresho ya mifumo ya kidijitali, EWURA itaweza kufuatilia kwa karibu mnyororo mzima wa biashara ya mafuta na gesi asilia—kuanzia hatua ya uagizaji, usambazaji hadi uuzaji katika vituo vya mafuta na gesi.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza uwazi, kupunguza mianya ya udanganyifu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. Vilevile, matumizi ya mifumo ya kidijitali yatasaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wadau na kuongeza kasi ya maamuzi ya kiutendaji.

Kwa ujumla, juhudi hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya nishati inakuwa imara, shindani na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.

About the author

Alex Sonna