Featured Kitaifa

PROF. NAGU: TARURA ONGEZENI ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA

Written by Alex Sonna

 

Dodoma

‎Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu ameitaka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya barabara hususan kuepuka kutupa taka ngumu kwenye mitaro ya maji.

‎Prof. Nagu amesema utupaji wa taka ngumu kwenye mitaro ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kusababisha mitaro kuziba hivyo kuzuia mtiririko wa maji na kuhatarisha usalama pamoja na uimara wa barabara.

‎Ametoa kauli hiyo alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Taasisi zake katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo Nanenane 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma.

‎Prof. Nagu ameihimiza TARURA kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara ikiwemo mitaro ya maji ili kujenga utamaduni wa pamoja wa kuitunza na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na serikali unakuwa na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.

About the author

Alex Sonna