Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amekitaka Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT) kutokuwa chama cha harakati, bali kutumia nafasi yake katika kutoa ushauri, kupatanisha jamii, kulea watoto na vijana, pamoja na kuhifadhi mila na desturi za Kitanzania.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo Agosti 29, 2026, katika Ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa CCWWT kwa mwaka 2026, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Amesema wazee wana nafasi ya kipekee katika jamii ya Kitanzania kutokana na heshima na hadhi waliyonayo, akieleza kuwa wamekuwa walinzi wa mila na desturi, washauri, wapatanishi na walezi wa watoto, vijana na jamii kwa ujumla.
“Wazee mna kazi kubwa na ya msingi ya kuhifadhi mila na desturi za Kitanzania, kuwa washauri na wapatanishi wazuri katika jamii, ikiwa ni pamoja na walezi wa jamii ya Kitanzania, hivyo, tekelezeni majukumu ya chama chenu kwa mujibu wa katiba yenu,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua wazee kama rasilimali na hazina kubwa katika maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa uwepo wa Tanzania kama taifa ni kielelezo cha mchango mkubwa uliotolewa na wazee katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Prof. Shemdoe amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha ya wazee nchini, sambamba na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa makundi yote bila ubaguzi. Ametaja miongoni mwa hatua hizo kuwa ni kuwekwa kwa mifumo ya kisheria inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma, ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya Mwaka 2023.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Mahundi, amesema Tanzania imefikia hatua ilipo leo kutokana na mchango mkubwa wa wazee ambao ni tunu ya taifa.
Amesema wazee wamejenga familia, wamelea watoto, wamefundisha vijana, wamejenga taasisi na kulitumikia taifa, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi. Kwa msingi huo, amesema taifa linapaswa kutumia ipasavyo maarifa, uzoefu na hekima walizonazo wazee kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza kwa niaba ya wazee, Katibu Mkuu wa CCWWT, Bw. Flavianus Lughuyu, amesema licha ya wazee kuacha alama kubwa katika historia ya taifa, bado kuna haja ya kujenga mifumo imara ya kuwaenzi na kutambua mchango wao.
Amesema historia na uzoefu wa wazee vinapaswa kutumika kama nyenzo ya kujenga maadili kwa vijana, ili kutambua kuwa kulitumikia taifa kwa uaminifu kuna thamani hata baada ya mtu kustaafu.
Mkutano huo umebeba Kaulimbiu isemayo: “Wazee ni Tunu, Tuwatunze kwaMaendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.”
Kaulimbiu hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, sambamba na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2024.



