Featured • Kitaifa

TANZANIA KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA BORA YA UWEKEZAJI KATIKA HUDUMA ZA BENKI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na Afisa Mtendaji Mkuu wa China Dasheng Bank, Bw. Xu Yueliang, baada ya kumalizika kwa mkutano wao ulioangazia ushirikiano wa maendeleo, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akisisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria katika Uwekezaji, wakati wa Mkutano na  Afisa Mtendaji Mkuu wa China Dasheng Bank, Bw. Xu Yueliang, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza Mkutano kati yake na Afisa Mtendaji Mkuu wa China Dasheng Bank, Bw. Xu Yueliang, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo alisema Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)

Na. Peter Haule na Abdul Madenge, WF, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Tanzania imeweka  mazingira mazuri ya Uwekezaji ili kuchochea maendeleo yenye tija kwa wawekezaji na watanzania kwa ujumla.

Mhe. Balozi Omar ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa China Dasheng Bank, Bw. Xu Yueliang, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Omar, alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Wawekezaji katika kuhakikisha uwekezaji unakuwa na manufaa na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, Bw. Yueliang alisema China Dasheng Bank inalenga kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuimarisha sekta ya fedha, kuchochea uwekezaji na kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia huduma za kibenki na suluhisho mbalimbali za kifedha.

Alisema benki hiyo imejipanga kuwezesha uwekezaji kutoka China kwa kusaidia kampuni za China zinazotarajia kuanzisha au kupanua shughuli zake nchini kupata ufadhili na huduma za miamala zitakazorahisisha shughuli zao za biashara.

Vilevile alisema kuwa benki hiyo inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kifedha kati ya Tanzania na China kwa kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa nchi.

Aliongeza kuwa benki hiyo itasaidia biashara ya kimataifa kupitia huduma za fedha za biashara, zikiwemo barua za dhamana za malipo (letters of credit), dhamana za benki, huduma za fedha za kigeni na malipo ya kuvuka mipaka.

Bw. Yueliang alisema China Dasheng Bank iko tayari kutambua na kusaidia fursa zenye tija katika sekta za kimkakati, zikiwemo viwanda, usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa, kilimo, nishati na miundombinu.

Alieleza kuwa benki hiyo itaendelea kutafuta fursa za kufadhili miradi yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, ajira na shughuli za kiuchumi.

China Dasheng Bank Limited ni benki ya ndani iliyoanzishwa Septemba 2017 chini ya Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002 (Companies Act, 2002, Cap. 212). Benki hiyo ilipewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Novemba 2018 na kuanza rasmi shughuli zake.

Bw. Yueliang alisisitiza kuwa benki hiyo inathamini fursa ya kujenga uhusiano wa karibu na Wizara ya Fedha na iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono maendeleo ya biashara, ukuaji wa uchumi na ujumuishaji wa kifedha nchini.

About the author

Alex Sonna