Featured • Kitaifa

CHATANDA: “WANAWAKE WAKIPEWA NAFASI NA KUAMINIWA WANAWEZA KUFANYA MAKUBWA”

Written by Alex Sonna

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Ndg. Mary Pius Chatanda (MCC), amesema wanawake wakipewa nafasi, kuaminiwa na kuwezeshwa wanaweza kufanya makubwa katika maendeleo ya nchi.

Akizungumza tarehe 29 Septemba 2026 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Dumila, Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya UWT Kitaifa, Chatanda amesema kuongezeka kwa wanawake katika nafasi za maamuzi kwenye siasa, elimu, biashara na taaluma ni ishara ya uwezo wao katika utumishi wa umma na jamii.

Chatanda amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mfano wa mwanamke aliyepewa nafasi na kuaminiwa, akieleza kuwa ni Mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa CCM na Rais mwanamke aliyechaguliwa kwa sanduku la kura. Aidha, amesema Dkt. Samia Suluhu Hassan ametajwa mara tatu miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo nchini.

Amesema mafanikio na mchango wa wanawake katika maendeleo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuwapa nafasi, kuwaamini na kuwawezesha ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Hata hivyo, Chatanda amesema bado kuna haja ya kuongeza jitihada za kuwawezesha wanawake na wasichana, akibainisha kuwa baadhi yao bado wanakatishwa ndoto zao mapema kutokana na vikwazo vya kiuchumi na ukatili wa kijinsia, huku wanawake wenye mchango mkubwa wakikosa fursa ya kusikika kikamilifu katika meza za maamuzi.

About the author

Alex Sonna