Na OWM-TAMISEMI
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) imejipanga kikamilifu kuwahudumia wananchi wote watakaojisajiliwa katika Bima ya Afya kwa wote kwa usawa na huduma bora kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utoaji wa huduma bora za afya ngazi ya msingi inayojumuisha zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri na Hospitali zenye hadhi ngazi ya wilaya.
Hayo yamebainishwa Oktoba 22, 2026 na Naibu Waziri OWM-TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt, Jafar Seif kwa niaba ya Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, wakati wa hafla ya kuanza usajili wa Bima ya Afya kwa wote awamu ya pili iliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara.
Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa ni Mhe. Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Afya, Dkt. Seif amesema mpaka sasa vituo vya kutolea huduma za afya 7,986 ikijumuisha hospitali za halmashauri 183, hospitali zenye hadhi ngazi ya wilaya 12, vituo vya afya 1,101 na zahanati 6,693 zimejengwa na zinatoa huduma katika halmashauri zote nchini na wananchi wanapata huduma za afya kikamilifu.
Amesema kutokana na hali hiyo OWM-TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya afya pamoja na Wizara nyingine, Idara na Taasisi mbalimbali kufanikisha usajili wa wananchi wenye uwezo wa kujilipia pamoja na wale wasio na uwezo ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanasajiliwa na kupata Huduma bora za Afya.
Ameongeza kuwa Wizara yake ina jukumu la kuhakikisha kuwa elimu na taarifa sahihi kuhusu mpango huo inawafikia wananchi na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuwasimamia watendaji ngazi za mikoa na halmashauri kutoa elimu hiyo kwa lugha inayoeleweka.
“Hakuna kaya isiyostahili kujisajili na Bima ya Afya kwa Wote, utaratibu utatumika kuzitambua kaya maskini na wale wenye uwezo wa kujigharamia waelimishwe kwa lugha inayoeleweka,” amefafanua Dkt. Seif.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, OWMI- TAMISEMI , Dkt. Rashid Mfaume akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu OWM- TAMISEMI, Bw. Adolf Ndunguru amesema mpaka sasa Sekretarieti zote za Mikoa 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 zimejengewa uwezo kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na zinaendelea vema na usajili wa wananchi na utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi waliosajiliwa katika mpango wa Bima ya Afya kwa wote awamu ya kwanza,.
Aidha, amesema OWM -TAMISEMI ina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 wa kusimamia na uratibu wa Bima ya Afya ya jamii katika sekta isiyo rasmi kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (Community Health Fund -CHF), hivyo wananchi waliokuwa wanahudumiwa na Mfuko wa Afya ya Jamii sasa wanahamia kwenye Bima ya Afya kwa Wote, na watahudumiwa kwa uzoefu huo, kwa ubora unaostahili, bila ya upendeleo na Changamoto zilizobainika katika Utekelezaji wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) zitatumika kama fursa za kuboresha zaidi utendaji na usimamizi wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Dkt. Mfaume ameeleza kuwa uzinduzi wa usajili wa Bima ya Afya kwa Wote awamu ya pili kitaifa mkoani Mtwara umeaenda sambamba na ngazi ya mikoa Tanzania Bara ukisimamiwa na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa.
Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya sabasaba mkoani Mtwara ilikwenda sambamba na zoezi la usajili wa wananchi katika mpango wa bima ya afya kwa wote ambapo wananchi waliofika viwanjani hapo waliosajiliwa na kupatiwa kadi zao za bima hiyo.
