Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) unashiriki Onesho la Nne la Kitaifa la Utamaduni kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake na Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja nchini.
Katika onesho hilo, wataalamu wa PBPA wanatoa maelezo kuhusu namna Wakala unavyoratibu uagizaji, upokeaji na uwasilishaji wa bidhaa za mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta ya ndege.
Wananchi wanaotembelea banda la PBPA pia wanaelimishwa kuhusu mchango wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja katika kuhakikisha bidhaa za mafuta zinapatikana nchini kwa uhakika, kwa wakati na kwa gharama shindani.
Aidha, PBPA inatoa elimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Upatikanaji wa Taarifa (SCADA), unaotumika kufuatilia ushushaji wa mafuta kutoka melini hadi kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta.
Ushiriki wa PBPA katika onesho hilo ni sehemu ya jitihada za Wakala kuimarisha mawasiliano na wananchi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu shughuli zake na mchango wake katika usalama wa upatikanaji wa nishati nchini.
PBPA imewakaribisha wananchi kutembelea banda lake ili kupata elimu, kuuliza maswali na kufahamu zaidi kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja.
