Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 5,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
SERIKALI imetangaza mkakati mpya na madhubuti wa kupunguza kiwango cha upotevu wa maji nchini, ikiahidi kuimarisha usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya wahujumu wa miundombinu ya maji.
Hayo yamebainishwa leo Mei 5, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, juhudi kubwa zitaelekezwa katika kudhibiti upotevu wa maji unaotokana na uzembe, miundombinu chakavu na vitendo vya wizi. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika huku ikilinda uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta hiyo.
“Miongoni mwa maboresho yatakayotekelezwa ni matumizi ya mifumo ya usomaji mita kwa njia ya kielektroniki, ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi za matumizi ya maji na kupunguza mianya ya upotevu.”amesema Aweso
Aidha, Serikali itaanzisha na kuimarisha mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji wa mtandao wa maji (smart water management system) utakaowezesha kubaini kwa haraka uvujaji au hitilafu katika mabomba.
Hata hivyo Wizara imepanga kuongeza kasi ya ukarabati wa miundombinu ya maji, hususan mabomba yaliyochakaa ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha upotevu. Sambamba na hilo, ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla utaendelea kuimarishwa ili kudhibiti matumizi na kuongeza uwajibikaji kwa watumiaji.
Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaohusika na uharibifu wa miundombinu au wizi wa maji. Imeonya kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa na wahusika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria bila upendeleo.
” Wizara imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa miradi mipya ya maji inajengwa kwa kuzingatia ubora, uimara na uwezo wa kuhimili changamoto za kimazingira ili kupunguza hasara za baadaye.”amesema
Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya maji na kuleta matumaini mapya kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.