Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho (Mb), amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali (SUMAJKT) kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana hapa nchini.
Mhe. Nyansaho ameyasema hayo Julai 06, 2026 alipotembelea banda la JKT kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. JK Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mhe. Nyansaho amefafanua kuwa Kampuni tanzu za SUMAJKT zimekuwa zikitoa mchango mkubwa wa kupunguza ombwe la ajira kwa vijana hapa nchini, akitolea mfano Kampuni ya usafi na Unyunyizi dawa (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Company Limited), ambayo imetoa ajira kwa vijana zaidi ya 4000 wa kitanzania.
Kando na hilo, Mhe. Dkt. Nyansaho amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ya Ulinzi na Uzalishaji Mali, katika kuhakikisha Taifa linakuwa salama na Wananchi wanatekeleza majukumu yao kwa amani.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwataka wananchi kutembelea banda la JKT ili kufahamu shughuli zote zinazotekelezwa na Jeshi hilo kupitia Vikosi, Makambi, Shule, Chuo na huduma na biashara zinazofanywa na kampuni Tanzu za SUMAJKT.
