Featured Michezo

GSM AWEKA BILIONI 15 KUSUKUMA USAJILI YANGA, KAMWE AFUNGUKA MALENGO YA MSIMU MPYA

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog

Klabu ya Yanga SC imeweka wazi ukubwa wa maandalizi yake kuelekea msimu wa 2026/27 baada ya kutangaza kuwa mfadhili wake mkuu, Ghalib Said Mohamed (GSM), ametenga takribani Sh bilioni 15 kwa ajili ya usajili wa wachezaji, hatua inayodhihirisha dhamira ya klabu hiyo ya kuendelea kutawala soka la ndani na kufanya makubwa katika mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema mfadhili huyo amempa uhuru Rais wa klabu hiyo, Eng. Hersi Said, kutafuta wachezaji wenye ubora bila kuwa na hofu ya upatikanaji wa fedha.

“Rais wetu Eng. Hersi alizungumza na mfadhili wetu GSM kuhusu usajili wa msimu huu. GSM alimweleza wazi kuwa atafute wachezaji wanaohitajika, fedha za kuwasajili zipo,” amesema Kamwe.

Amesema uwekezaji huo umeifanya Yanga kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania saini za wachezaji wanaowahitaji, huku akifichua kuwa klabu hiyo iliwahi kupambana kumsajili mchezaji mmoja aliyekuwa akihitajika na GSM, lakini mazungumzo hayakufikia makubaliano kutokana na msimamo wa mchezaji huyo.

Kamwe amesema Yanga imejipanga kujenga kikosi chenye ushindani mkubwa katika kila nafasi, hususan safu ya ushambuliaji, ili kuhakikisha timu hiyo inakuwa na uwezo wa kupambana katika mashindano yote itakayoshiriki.

Amesema mashabiki wa Yanga wanapaswa kutarajia ushindani mkali wa nafasi za mbele kutokana na uwepo wa washambuliaji nyota akiwemo Clement Mzize, Peter Shalulile, Erick Mwijage, Cheikh Ibrahim Touré, Maxi Nzengeli na Allan Okello.

“Watu wanauliza washambuliaji wote hao watachezaje, lakini sisi tunataka kuwa na kikosi kitakachoshinda kila mashindano. Kutakuwa na mechi ambazo wote wataweza kuanza pamoja kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi,” amesema 

Katika hatua nyingine, Kamwe ametoa taarifa njema kuhusu hali za majeraha za washambuliaji Clement Mzize na Dickson Job, akisema awali walitarajiwa kurejea uwanjani mwezi Desemba, lakini maendeleo ya matibabu yao yanaonyesha wanaweza kuanza kucheza mapema zaidi, huenda kuanzia Oktoba.

Amesema kurejea kwa wachezaji hao kutazidi kuimarisha kikosi cha Yanga, ambacho tayari kimefanya usajili mkubwa kwa lengo la kutetea mataji ya ndani na kufikia mafanikio makubwa katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kwa maandalizi hayo makubwa na uwekezaji wa kiwango cha juu, Yanga inaingia msimu mpya ikiwa na matarajio makubwa ya kuendelea kuwa miongoni mwa klabu zenye ushindani mkubwa zaidi nchini na barani Afrika.

About the author

Alex Sonna