Na.Alex Sonna,Mzalendo blog
Klabu ya Yanga imetangaza kuwa Tamasha la Yanga Day 2026 litakuwa la kipekee, likiwa na burudani, maonesho ya kikosi kipya na mchezo maalumu wa Siku ya Mwananchi, huku mashabiki wakitarajiwa kushuhudia kwa mara ya kwanza nyota wapya waliosajiliwa kuelekea msimu wa 2026/27.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema mpinzani wa mchezo huo utakaochezwa Agosti 9, 2026, katika Uwanja wa Uhuru, atatangazwa rasmi mara baada ya Mkutano Mkuu wa klabu utakaofanyika Agosti 2
Kamwe amesema tamasha la mwaka huu limeongezeka hadhi kutokana na usajili mkubwa uliofanywa na klabu, hatua inayowapa mashabiki nafasi ya kujionea kikosi kipya kilichoundwa kwa lengo la kutetea ubingwa wa ndani na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
“Tumejipanga kuhakikisha Yanga Day ya mwaka huu inakuwa ya kipekee. Mashabiki watapata fursa ya kuwaona kwa mara ya kwanza wachezaji wetu wapya pamoja na kufurahia burudani mbalimbali zitakazofanya tamasha hili kuwa la kukumbukwa,” amesema Kamwe.
Kuhusu tiketi, amesema Royal Ticket itauzwa kwa Sh 300,000 na itawapatia mashabiki huduma maalumu zikiwemo jezi mpya ya msimu iliyosainiwa na mchezaji watakayemchagua, usafiri wa kwenda na kurudi kutoka Serena Hotel pamoja na chakula wakati wa mapumziko.
Aidha, tiketi za VIP zitauzwa kwa Sh 100,000, huku tiketi za Mzunguko zikiuzwa kwa Sh 20,000 ili kuwapa mashabiki wengi zaidi nafasi ya kushiriki tamasha hilo.
Yanga inaendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea msimu mpya, huku matarajio ya mashabiki yakiongezeka siku hadi siku wakisubiri kuona sura mpya ya kikosi hicho, kitakachozinduliwa rasmi katika tamasha la Yanga Day 2026.