NA OR-TAMISEMI
IMEELEZWA kuwa kujengwa kwa daraja la Berega lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro limewaondolea adha wanawake na watoto ambao walikuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameyasema hayo leo Agosti 2, 2024 mbele ya Mhe. Rais Samia kwenye ziara yake alipokuwa akizindua daraja la Berega wilayani humo.
Amesema daraja Daraja hilo ni kiungo muhimu sana kwa kuwa linaunganisha Mikoa miwili wa Morogoro na Tanga kwenye Wilaya ya Kilindi ambapo eneo hilo lilikuwa likikosa mawasiliano kwa mwaka mzima kutokana na maji kujaa na kusababisha wananchi kushindwa kuvuka upande wa pili kupata huduma za kijamii ikiwamo za afya.
“Kwa kipindi kirefu wananchi wamepata shida, wameshindwa kusafirisha bidhaa zao kwenda sokoni lakini wamepoteza maisha yao kutokana na maji kujaa msimu wa mvua na kupelekea wananchi wa Kilosa na Kilindi kushindwa kuwasiliana na kukosa fursa za msingi za kibiashara, kijamii na kiafya.”
“…Lakini Mhe. Rais kwa kuliona hilo ukatoa sh.Bilioni saba ambazo zimewezesha ujenzi wa daraja hili lenye urefu wa Mita 140 na linalounganisha Kata za Berega wilayani Kilosa na Makuyu wilayani Kilindi kuanzia leo hii adha kwa wananchi hawa itakuwa ni historia Mhe. Rais tunakushuru sana kwa kujali shida za watanzania,”amesema Mhe. Mchengerwa.