Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema atagharamia gharama za masomo kwa watoto 10 wa kata ya Mbwara wilayani Rufiji katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA, ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wenyeji kuwapeleka watoto wao katika chuo hicho wilayani Rufiji.
Waziri Mchengerwa ametangaza kuchukua hatua hiyo wakati wa mikutano yake ya adhara na wakazi wa kata ya Mbwara alipotembelea vijiji vya Nambunju, Mbwara na Nyamwage katika kata hiyo kwa lengo la kuhimiza wananchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya barabara, maji, afya na elimu.
Mhe. Mchengerwa amesema, licha ya uwepo wa chuo hicho cha VETA wilayani Rufiji ambacho kimejengwa kwa fedha nyingi za serikali, lakini mwitikio wa wananchi kuwapeleka watoto wao kupata elimu ya ufundi stadi katika chuo hicho umekuwa hafifu, hivyo ameamua kusomesha watoto 10 ikiwa ni sehemu ya kuwahimiza wakazi wa wilaya hiyo kutumia ipasavyo fursa ya uwepo wa chuo hicho.
“Wananchi wenzangu, nimepambana sana mpaka tumepata chuo chetu cha Mafunzo ya Ufundi stadi VETA lakini hampeleki watoto kupata elimu katika chuo hiki, hii si dalili nzuri kwani fursa hii ni yetu hivyo tuitumie kwa maendeleo yetu,” Waziri Mchengerwa alisisitiza.
Aliongeza kuwa “Sasa naombeni mnipe watoto 10 yatima wanaotoka katika familia duni, watoto hao nitawasomesha mwenyewe kwa kulipia gharama zote zitakazohitajika chuoni VETA,” Mhe. Mchengerwa aliahidi.
“Ninafanya hivi ili niwe mfano kwenu na nyinyi mshawishike kuitumia fursa hii ili watoto wetu wapate ujuzi, sasa tuwapeleke chuo ili kesho yao iwe yenye mafanikio” aliongeza Mchengerwa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa chuo hicho Mhandisi Julius Mwakasasa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi wilayani Rufiji kilianza kutoa mafunzo yake mwezi Mei 2024, na mpaka sasa kina jumla ya wanafunzi 16, licha ya kuwa na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 172.