Featured Kitaifa

DKT.BITEKO AWEKA JIWE LA MSINGI AFISI YA UHAMIAJI NA MAKAAZI YA ASKARI WILAYA YA MKOANI KUSINI PEMBA

Written by mzalendo

Pemba – Zanzibar

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kuyaenzi, kuyalinda na kuyaishi kwa dhamira ya dhati, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwani Waasisi wa Nchi  walifanya mapinduzi hayo ili kuwa na Taifa huru ambalo kila mtu anakuwa na hadhi, kuondoa dhuluma iliyokuwepo na kufanya wananchi kuishi kwa amani na furaha.

Amesema hayo tarehe 6 Januari 2024 wakati akizungumza na Wananchi katika Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba mara baada ya kuzindua Afisi ya Uhamiaji na Makaazi ya Askari wilayani humo.

“ Sisi Wananchi tunawajibu wa kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kuyaishi, kuyaheshimu,  kukuza uchumi wa nchi na kukuza uzalendo ili baada ya muda mrefu hata baada ya miaka 100 mbele, watakaokuja kusherehekea Mapinduzi haya wakute Zanzibar iliyobora zaidi na waseme Mapinduzi haya yalitufaa.” Amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa, moja ya tunu tuliyonayo ni mshikamano hivyo watu wasiruhusu mtu yoyote kuwagawanya kwa misingi yoyote ile, bali maendeleo yaunganishe watu wote na kwamba tofauti za vyama, dini na kabila visifanye watu wakae kwenye makundi bali kuunganisha watu kwa maslahi ya nchi na watanzania.

Amesema kuwa, nchi inapoenda kusherehekea Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe 12 Januari mwaka huu, watanzania wote waungane kuwaombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ili waendelee kuongoza vyema, kuimarisha ustawi wa Taifa na kuwaunganisha Watanzania.

Kuhusu Jengo hilo jipya la Afisi ya Uhamiaji katika Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba, Dkt, Biteko amesema kuwa ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani kabla ya Mapinduzi watu walinyimwa haki zao za kimsingi zikiwemo za uhamiaji kama vile kupata pasi ya kusafiria na hivyo Mapinduzi yamewezesha wananchi kupata uhuru wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi.

Ameongeza kuwa, Ofisi hiyo ya Uhamiaji wilaya ya Mkoani ilianza mwaka 1979 ikiwa ni ndogo lakini sasa kuna jengo la kisasa litakalowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Wilaya hiyo na viunga vyake, ikiwa ni kielelezo cha Mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amepongeza viongozi Wakuu wa nchi kwa juhudi wanazochukua ili wananchi wapate huduma bora ikiwa pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Vilevile amewapongeza  viongozi wa Idara ya Uhamiaji kwa usimamizi wa jengo hilo na kuiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuona namna ya kujenga jengo kama hilo katika wilaya mbalimbali nchini kwani  ni jengo la kisasa lililozingatia watu wenye mahitaji maalum, limechukua eneo dogo na kujengwa kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Jumanne Sagini amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema anayoyafanya kwa kwa vyombo vya usalama nchini ikiwemo kutoa vibali vya ajira, upandishaji vyeo, mafunzo, ulipaji madeni na kuwezesha vyombo vya usalama kwa kununua vitendea kazi.

Amesema kuwa, Idara ya Uhamiaji imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Idara hiyo kwani mwaka 2022/2023, Idara ililenga kukusanya shilingi bilioni 56.5 lakini ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 67.679 na mwaka huu wa fedha unaoendelea imekusudia kukusanya shilingi bilioni 75 lakini hadi  mwezi Desemba
ilikusanya bilioni 43.119 ambayo ni zaidi ya nusu ya malengo huku matarajio yakiwa ni kufikia malengo yaliyowekwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dkt. Islam Seif, amesema kuwa, Afisi hiyo ya uhamiaji ilianza kujengwa mwezi Agosti mwaka 2022 na kukamilika mwezi Novemba, 2023 huku akisema kuwa jengo hilo la kisasa litakidhi mahitaji ya sasa ikiwemo uwepo wa mifumo ya Tehama ambayo ni muhimu katika ufanyaji katika afisi hizo.

Amesema gharama za ujenzi wa Afisi hizo ni shilingi Bilioni 1 na milioni 53 huku akieleza kuwa jengo lililopo linaakisi gharama hizo.

Amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati Pemba ikiwemo kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa, mahoteli pamoja na afisi za kisasa.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi na pia kuboresha huduma mbalimbali za wananchi.

Amesema kuwa mafanikio mbalimbali yanayotokea sasa ni kutokana na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964 ambapo pia Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar uliasisiwa.

Amesema Idara hiyo inaendelea na ujenzi wa jengo jingine la Afisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo amepongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa maeneo ya ujenzi wa Afisi hizo.

About the author

mzalendo