Rais wa Jamhuri ya Kenya William Ruto amesisitiza umuhimu kwa mataifa ya Afrika kubadili mtazamo kuhusu uwekezaji, akieleza kuwa wakati umefika wa kuthamini na kuamini wawekezaji wa ndani ya bara hilo badala ya kuwapa kipaumbele wawekezaji kutoka nje pekee.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Jumanne, Mei 5, 2026, Ruto amesema bado kuna dhana iliyojengeka katika baadhi ya nchi za Afrika kuwa mwekezaji wa maana lazima atoke nje ya bara, hali ambayo imeelezwa kuwa inakwamisha ukuaji wa uchumi wa ndani.
Katika hotuba yake, Ruto alimtaja mfanyabiashara wa Tanzania, Rostam Aziz, kama mfano wa changamoto wanazokutana nazo wawekezaji wa ndani. Alisema Rostam alikumbana na vikwazo wakati akijaribu kuwekeza katika sekta ya gesi nchini Kenya, hadi ilipolazimu uingiliaji wake binafsi ili kupata suluhisho.
“Nilipewa taarifa kuhusu changamoto hizo, nikawaeleza Wakenya kuwa mwekezaji huyo ni mshirika wetu wa maendeleo na anapaswa kupokelewa kama sehemu ya Afrika,” amesema Ruto.
Ameeleza kuwa bara la Afrika lina fursa kubwa ya kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mshikamano, kuaminiana na ushirikiano wa ndani, badala ya kutegemea zaidi mitaji ya nje.
Ruto amesisitiza kuwa uwekezaji wa ndani unaweza kuwa nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, iwapo utawekewa mazingira rafiki na sera zinazounga mkono ukuaji wa sekta binafsi ndani ya bara.