Rais wa Jamhuri ya Kenya William Ruto amesema kampuni 500 kutoka Kenya zimewekeza takribani dola za Marekani bilioni 1.7 nchini Tanzania, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Mei 5, 2026, Rais Ruto amesema uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa ajira kwa maelfu ya wananchi pamoja na kuongeza mapato ya serikali.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya, akibainisha kuwa ushirikiano huo unaendelea kukua siku hadi siku.
Kadhalika, Rais Ruto amesema kuwa si Kenya pekee inayowekeza Tanzania, bali pia kampuni za Kitanzania zimeendelea kupanua uwekezaji wao nchini Kenya, jambo linaloonesha usawa wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
Akitolea mfano, amezitaja kampuni za Taifa Gas, Amson Group na Lake Gas kuwa ni miongoni mwa wawekezaji wa Kitanzania waliopanua shughuli zao nchini Kenya.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, uwekezaji huo umeendelea kukua kwa kasi na unatarajiwa kuongeza mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili
“Kampuni kutoka Tanzania pia zimewekeza Kenya na niliwaambia Wakenya kwamba mwekezaji kutoka Tanzania ni mshirika wetu; wanatuletea mtaji na fursa ambazo tungeweza kutumia muda mrefu kuzipata,” amesema Ruto.
Katika kusisitiza umuhimu wa kukubali uwekezaji wa ndani ya Afrika, Rais Ruto ameeleza kuwa aliwahi kukumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wananchi walipohoji uwekezaji wa Mtanzania nchini Kenya.
“Nilipompa mwekezaji Mtanzania kiwanda, kulikuwa na malalamiko. Niliwauliza, awali kilimilikiwa na Wafaransa, kwa nini hamkulalamika? Sasa kinapomilikiwa na Mwafrika mwenzetu ndipo mnahoji?” amehoji Ruto.