Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi Eng. Julius Msofe kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa- Pangani (Km 120.8), wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa maagizo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15th wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa- Pangani (Km 120.8), wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akisisitiza jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Mohamed Besta (kulia), wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mkange –-Tungamaa- Pangani (Km 120.8), wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Eng. Aloyce Matei (kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa- Pangani (Km 120.8), wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa – Pangani (Km 120.8), ukiendelea wilayani Pangani, mkoani Tanga.
PICHA NA WU
………..
Waziri wa ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuchelewa kwa ukamilishaji na kutotekelezwa kwa miradi ya barabara nchini kwa wakati na viwango vinavyotakiwa kunasababishwa baadhi ya Wataalam na Wasimamizi wa Miradi hiyo wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.
Ameyasema hayo Mkoani Tanga wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa – Pangani yenye urefu wa Km 120.8 ambayo inatekelezwa na Mkandarasi, China Railway 15 na kusema hajaridhishwa na hali ya usimamizi wa mradi huo ambao upo nyuma kwa asilimia kwa 19.2
Bashungwa amesema tayari ameanza kuchukua hatua kwa wataalam ambao wamekuwa sababu ya miradi kutotekelezwa kwa wakati kulingana na mikataba ambapo amemuondoa Mkurugenzi wa miradi ya TANROADS, Eng. Boniface Mkumbo.
“TANROADS niliwambia, nileteeni orodha ya barabara zote ambazo utekelezaji wake una sua sua lakini hii hamkuleta, sasa unajua kwanini nimemfukuza Mkurugezi wa miradi TANROADS, Eng. Boniface Mkumbo, ambaye alikuwa sehemu ya kusababisha haya” amesema Bashungwa.
Bashungwa amemtaka Kaimu Mkurugenzi mpya wa miradi ya TANROADS, Eng. John Malisa kuzunguka katika miradi yote ya barabara nchini na kumletea taarifa ya miradi yote inayo sua sua ili aweza kuchukua hatua.
Aidha, Bashungwa amamuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohammed Besta kuhakikisha kila Mradi unaotekelezwa uwe na Msimamizi na Meneja, ambao watakuwa katika maeneo ya miradi hiyo wakati wote mpaka mradi utakapokamilika.
“Gharama za ucheleweshwaji wa ujenzi wa Barabara ni kubwa kiuchumi kwa maendeleo ya wananchi hivyo Serikali haitavumilia mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza mradi kwa wakati kulingana na mkataba” amesema Bashungwa.
Kadhalika, Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohammed Besta kufanya usanifu wa kina wa Barabara ya Mkata – Kwamsisi yenye 36, ifikakapo Desemba 31 mwaka huu ili iweze kutengewa bajeti ya kujengwa kwa Kiwango cha lami.
Nae, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohammed Besta amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa maelekezo yake yanafanyiwa kazi ili kukamilisha miradi inayoendelea na kujenga miradi mipya.