Featured Kitaifa

UZINDUZI WA WIKI YA CHANJO KITAIFA KUFANYIKA MKOANI MANYARA

Written by mzalendoeditor

Na. Catherine Sungura, Dodoma

Wizara ya Afya inaendelea  kuikinga jamii ya Watanzania dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo ambayo ni Kifua kikuu, Donda Koo, Kifaduro, Polio, Surua, Rubella, Pepo punda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo, Kichomi, Kuhara na Saratani ya shingo ya kizazi.

Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kwenye tamko lake la kuelekea maadhimisho ya wiki ya Chanjo duniani ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika kuanzia  tarehe 24 hadi 30 Aprili, 2023, yakiwa na  kauli mbiu “ Tuwakinge wote Kwa  Chanjo ”  ikienda sambamba na ujumbe usemao  “Jamii Iliyopata Chanjo, Jamii Yenye Afya”. 

“Wizara ya Afya iliweka huduma ya Chanjo kuwa kipaumbele cha kwanza kati ya vipaumbele vyake kumi kwa mwaka 2022/2023. Katika kufikia malengo ya kipaumbele hiki, Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya huduma za afya ili kuhakikisha walengwa wote wanapata Chanjo”.ameeleza Prof. Nagu.

Prof. Nagu amesema kuwa Shirika la Afya Duniani liliweka maadhimisho ya wiki ya Chanjo kila ifikapo wiki ya mwisho ya mwezi Aprili.” Wiki ya Chanjo Duniani ni wiki muhimu katika kuhamasisha Wananchi wote Ulimwenguni ili wanaelewe  umuhimu wa Chanjo na athari zinazotokana na kukosa Chanjo”.

Aidha, Prof. Nagu amezitaja athari za kukosa chanjo ni pamoja na ulemavu wa kudumu na vifo hususani kwa watoto chini ya miaka mitano. “Katika kuhakikisha kuwa jamii inaelewa umuhimu wa chanjo hapa nchini, kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine Duniani katika maadhimisho haya”.

Hata hivyo prof. Nagu ametoa wito  kwa Wanahabari, Wananchi, Viongozi wa Jamii na Viongozi wa madhehebu ya Dini kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusu umuhimu wa Chanjo, kuwaelimisha wazazi na walezi na kuwaelekeza kupeleka walengwa kwenye Vituo vya kutolea Huduma za Afya ili kupata Chanjo. Uzinduzi wa wiki ya chanjo Kitaifa yatafanyika mkoani Manyara tarehe 24 Aprili,2023.

About the author

mzalendoeditor