Featured Kitaifa

DAKTARI BINGWA WA MOYO AONYA MADHARA YATOKANAYO NA KUACHA KUTUMIA DAWA ZA PRESHA

Written by mzalendoeditor

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa akiwatambulisha wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wananchi wa Chalinze kabla ya kuanza kwa upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari unaofanyika  katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze ya Msoga Mkoani Pwani.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akitoa elimu ya magonjwa ya moyo na namna ya kuyaepuka kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kabla ya kuanza kwa upimaji wa magonjwa ya moyo na sukari unaofanywa na wataalam wa JKCI katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga Mkoani Pwani.

Meneja wa kampuni ya waingizaji wa wasambazaji wa dawa za binadamu ya Sun Pharma nchini Tanzania Sapajan Sorajam akiwaambia wananchi dawa ambazo kampuni hiyo itazitoa bila malipo kwa watu watakaokutwa na magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu wakati wa upimaji uliyofanywa na wataalam wa JKCI kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze  katika Hospitali ya Msoga Mkoani Pwani.

Afisa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akitoa elimu ya lishe kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze waliofika katika Hospitali ya Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari unaofanywa na wataalam wa afya kutoka JKCI.

Afisa Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Isimbuye akiwagawia vipeperushi vinavyoelezea huduma za matibabu zinazotolewa na JKCI wananchi waliofika katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo unaofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI katika Halmashauri hiyo iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Wananchi wa Halmashauri ya Chalinze wakisikiliza mada mbalimbali za afya ya moyo zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa upimaji maalum unaofanywa kwa wananchi hao kwa ajili ya kuchunguza magonjwa ya moyo na kisukari unaofanyika katika Hopitali ya  Halmashauri hiyo iliyopo Msoga  wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mwanahela Ally akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya hiyo iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Chalinze.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paul Josephat akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi aliyefika katika Hospitali ya halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Chalinze.

Mfamasia kutoka Kampuni ya uagizaji na usambazaji dawa za binadamu ya Sun Pharma Simon Salum akimuelezea matumizi ya dawa mwananchi aliyekutwa na tatizo la sukari wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wananchi wa Hamashauri ya Chalinze katika Hospitali ya Msoga. Kampumi ya Sun Pharma imetoa dawa bila malipo kwa wananchi wote waliokutwa na magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na moyo.

Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jackline Mathew akimuelezea mwananchi mfumo bora wa maisha wakati wa upimaji wa magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu unaofanywa na wataalam wa afya kutoka taasisi hiyo kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amanda Anyoti akimshauri mwananchi umuhimu wa kutumia dawa za kisukari wakati wa upimaji uliyofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.

 Fundi sanifu wa moyo (Mteknolojia) kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria akimpima mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiograph – ECG) mwananchi wa Halmashauri ya Chalinze wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi hao jana katika Hospitali ya Msoga Mkoani Pwani.

 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwetwe (JKCI) Mohamed Alyoce akimpima mwananchi wa Halmashauri ya Chalinze kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi hao jana katika Hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabella Seif akifanya mahojiano na wananchi wa Halmashauri ya Chalinze waliofika katika upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari uliofanywa na wataalam wa afya kutoka JKCI jana katika Hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo Msoga iliyopo Mkoani Pwani. 

Picha na: JKCI

………………………………………………

Na Mwandishi Maalum – Chalinze, Pwani

Kuacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu (Presha) kunaweza kusababisha madhara makubwa mwilini ikiwa ni pamoja na moyo na figo kutokufanya kazi vizuri kama inavyotakiwa, ugonjwa wa kiharusi, vifo vya ghafla na misuli yad amu ya moyo kutanuka. 

Onyo hilo limetolewa leo  na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Peter Kisenge wakati akiongea na wananchi waliofika kupima magonjwa ya moyo na kisukari  katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wataalamu wa JKCI wako katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuwapima wananchi na kutoa uelewa wa magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo  na lishe bora.

“Siku ya jana tumefanya upimaji kwa watu 185 wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu lakini wameacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa dawa, kutokuwa na uwezo wa kununua dawa na kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya dawa. Kuna ambao tumewakuta misuli yao ya damu ya moyo imetanuka hii yote ni madhara ya kuacha kutumia dawa za presha”,. 

“Tumewaanzishia dawa na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya dawa kwani wengi wanatumia dawa na kuziacha hawajui kuwa matumizi ya dawa za presha ni maisha pia tumewaambia madhara wanayoweza kuyapata pale watakapoacha kutumia dawa za presha”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema huduma wanazozitoa katika upimaji huo ni za kupima urefu na uzito, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu, kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi na kuangalia jinsi moyo  unavyofanya kazi, kutoa elimu ya lishe bora kwa afya ya moyo na matumizi sahihi ya dawa za moyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata kwani wameweza kupima vipimo vya moyo, kisukari pamoja na kupewa dawa bila malipo yoyote yale.

“Nilikuwa nikilala usiku nasikia moyo wangu unadunda kwa nguvu nikapata hofu kuwa ninatatizo la moyo, baada ya kusikia wataalamu wa moyo wako hapa nimekuja kupima na kukutwa moyo wangu hauna shida ila nina tatizo la presha ambayo iko juu nimeandikiwa dawa za kwenda kutumia “, alishukuru mzee Salum Funua mkazi wa Msoga.

Juliana Selemani mkazi wa Chalinze Mbwilingu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema anatatizo la presha  kwa muda wa miaka mitatu na huwa anatumia dawa lakini pale anapojisikia kuwa na naafuu anaacha kuzitumia.

“Leo hii  baada ya daktari kunifanyia vipimo amenikuta na tatizo la kutanuka kwa misuli ya moyo ameniambia tatizo hii limetokana  na kuacha kutumia dawa kwani presha imeuumiza moyo wangu. Baada ya kupewa elimu hii sintaacha kutumia dawa, ninawashauri wagonjwa wa presha kama mimi wasiache kutumia dawa hata pale wanapojiona kuwa na naafuu”, alisema Mama Juliana. 

Kwa upande wake fundi sanifu wa moyo (Technician) kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria alisema upimaji huo umesaidia kuweza kutumika kwa mashine nzuri na ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo ambayo ilikuwepo katika Hospitali hiyo.

“Hospitali hii inamashine nzuri ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiogram – ECG) lakini hawakuwa wanaitumia hii ni kutokana na kutokuwa na utaalamu nayo, nimeifungua mashine hii nimeiset program na tumeitumia kuwapima wagonjwa”,. 

“Nimewafundisha jinsi ya kuitumia na hapa tulipo tunashirikina na  wataalamu wa hapa kuwapima wagonjwa kwa kufanya hivyo kutasaidia wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hii kuweza kupata huduma hii ya vipimo”, alisema Jasmin.

Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa alishukuru kwa huduma inayotolewa kwa wananchi ya kupimwa magonjwa ya moyo na kisukari pamoja na wafanyakazi wa hospitali ya halmashauri hiyo kufundishwa  jinsi ya kutumia mashine ya  mfumo wa umeme na moyo pamoja na kuwapima wagonjwa.

Upimaji huo wa siku mbili unafanywa na wataalamu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga, kampuni ya dawa za binadamu ya Sunpharma ambayo inatoa dawa kwa watu wanaokutwa na tatizo la moyo, sukari, maumivu, upungufu wa damu na kampuni ya ulinzi ya K4 Security ambao wanahakikisha uwepo wa usalama kwa wananchi pamoja na mali zao.

About the author

mzalendoeditor