Featured Kitaifa

MSIGWA-‘SERIKALI IPO KWENYE MAZUNGUMZO NA WAWEKEZAJI JUU YA UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO

Written by mzalendoeditor

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Gerson
Msigwa akizungumza  wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma
nchini  katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga wakiendelea na
kikao chao

Sehemu ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma wakiwa kwenye Bandari ya Tanga wakati wa ziara hiyo

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.

SERIKALI
ipo na mazungumzo na  wawekezaji juu ya mpango wa ujenzi wa Bandari
mpya ya Bagamoyo  mkoani Pwani ili kusogeza huduma karibu na wananchi na
hivyo kuchangia kukuza pato la Taifa na wananchi kwa ujumla.

Hayo
yalisemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari
Maelezo,Gerson Msigwa wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na
Taasisi za Umma nchini  katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga
wakiendelea na kikao chao

Alisema kwa sasa wamerejesha mazungumzo hayo baada ya Rais Samia Suluhu kupitia serikali yake
ya awamu ya sita kuona ni vyema wakarejesha mazungumzo hayo na
kukubaliana maeneo serikali itayoona ina maslahi nayo pamoja na
wawekezaji ili wautekeleze mradi huo. 
Alisema
huo mradi huo ni mkubwa na wakifanikiwa kuutekeleza  utasaidia
kuchochea kasi ya maendeleo na hivyo kuchangia pato la wananchi na Taifa
kwa ujumla ikiwemo kufungua milango ya uwekezaji hapa nchini. 
Alisema
sio Bandari bali patajengwa Viwanda, kwasababu eneo hilo wanakusudia
kulifanya liwe kanda maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo  pale panajengwa
bandari, Viwanda, eneo la makazi ,maduka makubwa na sehemu nyingi za
kibiashara ikiwemo ujenzi wa viwanda takribani 1000 na hivyo itawezesha
kuwa kanda maalumu ya viwanda. 
Akizungumzia
ujenzi wa Bandari unaoendelea katika Mikoa ya Dar es Salaam,  Tanga na
Mtwara Msigwa alisema wamewapeleka maafisa habari wa serikali ili waone
kazi kubwa inayotekelezwa na serikali ili wananchi wanapotaka kujua nini
serikali inafanya katika fursa ya uchumi wa bluu  ili wajue kwamba kuna
kazi kubwa inayofanyika. 
“Niwaambie kwamba hii moja kati ya kazi kubwa ambazo zinafanyika hapa Tanga lakini pia
tunafanya kazi kama hizi kwenye maziwa yetu ikiwemo Kigoma, Kalema kule
kwenye ziwa Tanganyika,  Ziwa Victoria pia pale Mwanza tumejenga cholezo
kubwa na ujenzi wa meli unaendelea kule kwa hiyo kuna kazi nyingi
serikali inafanya,kwenye maeneo haya na tungependa maafisa habari wetu
wajionee wao wenyewe na kupeleka huu ujumbe mzuri kwa wananchi,
“Alibainisha Msigwa. 
Akizungumzia
miundombinu ya reli Msigwa alisema serikali imefanya kazi kubwa ya
kuhakikisha treni zinarejea Mkoani Tanga mpaka Arusha ambapo hivi sasa
kazi inayokwenda kufanyika ni ya kuimarisha miundombinu hiyo na kuona
namna bora ya kuja na reli nzuri zaidi. 
Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mhandisi
wa bandari ya Tanga Hamis Omari Kipalo amesema kwa upande wa ujenzi wa
gati namba moja na namba mbili katika bandari hiyo umefikia asilimia 45
mpaka sasa. 
Mhandisi huyo alisema mradi wao kimkataba unatakiwa kukamilika tarehe 16 mwezi octoba mwaka huu. 
Baadhi
ya maafisa habari waliotembelea bandarini hapo wamesema ziara hiyo
imewasaidia kuona namna serikali ilivyojizatiti kwenye utekelezaji wa
miradi mikubwa ya maendeleo. 
David
Mwaipaja ni Afisa mahusiano na mauzo kutoka Watumishi Housing
Investment amesema kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika
bandari zetu ambazo zipo kwenye miradi ya kimkakati jambo ambalo
litakuwa chachu kwa maafisa habari kuchukua na kwenda kuisemea serikali
kwa wananchi ili mambo yasiyoonekana kiurahisi kwa wananchi basi yaweze
kuwafikia sawasawa na serikali inavyofanya. 
Upanuzi
wa ujenzi wa mradi wa gati za kisasa katika bandari nchini unatarajiwa
kufungua fursa za kibiashara ambapo ujenzi huo umefanyika katika Mikoa
ya Tanga,  Mtwara na Daresalaam. 
Kwa
upande wa bandari ya Daresalaam jumla ya shilingi trilioni moja nukta
mbili zinatarajiwa kutumika kwajili ya ujenzi wa gati sambamba na
kununua vifaa vitakavyorahisisha utoaji wa huduma ikiwemo upakuaji wa
shehena. 

About the author

mzalendoeditor