Featured Kitaifa

WANANCHI KIGOMA WATAKIWA KUTUNZA MIUNDOMBINU YA ANWANI ZA MAKAZI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akihutubia viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma kuhusu utekelezaji na uhamasishaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi leo mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma akielekeza jambo wakati akikagua utekelezaji wa Anwani za Makazi katika mitaa ya Simu na Lumumba leo mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akisisitiza jambo kwa wakusanya taarifa wa Anwani za Makazi, wa kwanza kulia Bi. Ummy Maulidi na Selemani Issa wakati akikagua utekelezaji wa Anwani za Makazi katika mitaa ya Simu na Lumumba leo mkoani Kigoma.  Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Bi. Ester Mahawe. 

Picha na Jumaa Wange

…………………………………

Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Kigoma

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kutunza miundiombinu ya Anwani za Makazi kwa manufaa ya mkoa na nchi kwa ujumla.

Akizungumza leo mkoani humo, wakati akikagua utekelezaji na uhamasishaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Waziri huyo aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanatunza miundombinu iliyowekwa ambayo ni vibao na nguzo vyenye majina ya mitaa, namba zilizoandikwa au kubandikwa katika majengo yao kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi zaidi.

“Hizi namba ni kwa ajili ya manufaa ya wananchi, zimewekwa ili kurahisisha utoaji huduma mfano ikitokea mwananchi unahitaji huduma polisi basi unaweza kuwatajia namba na wakafika nyumbani kwako na kutoa msaada unaohitaji, lakini pia itasaidia kufikishiwa huduma zigine za maji, umeme na mawasiliano” Alisema Naibu Waziri Kundo

Alisisitiza “Tuchukulie miundombinu hii kwa umakini, nchi zilizoendelea mfano China, Marekani, Uswisi wao wamepiga hatua na hivyo na sisi lazima tujitahidi kufika huko lakini tutunze miundombinu hii na tuokoe fedha kwa ajili ya maendeleo yetu”.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Ester Mahawe alisema kuwa mkoa wake umetoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu faida na utunzaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi na watachukua hatua kwa wananchi watakaoharibu miundombinu hiyo.

“Naomba hawa wanaoharibu miundombinu hii niwachukulie hatua kwa kuwa haya ni maelekezo ya Mhe. Rais na sisi tutatekeleza kwa kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.” Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

About the author

mzalendoeditor