MKURUGENZI wa Petroli Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Bw.Gerald Maganga,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma kuhusu Bei Kikomo za bidhaa za Mafuta ya Petroli kuanzia siku ya Kesho April 6,2022.
MKURUGENZI wa Petroli Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Bw.Gerald Maganga,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitangaza Bei Kikomo za bidhaa za Mafuta ya Petroli kuanzia siku ya Kesho April 6,2022.
…………………………………….
Na Bolgas Odilo-DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetaja bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini kuwa zitaanza kutumika kuanzia kesho Jumatano April 6,2022.
Hayo yameelezwa leo April 5,2022 na MKURUGENZI wa Petroli Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Bw.Gerald Maganga,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu Bei Kikomo za bidhaa za Mafuta ya Petroli zinazoanza siku ya Kesho April 6,2022.
Bw.Maganga amesemam kuwa Bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli ,dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa Kupitia bandari ya Dar Es Salaam zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la 2 Machi ,2022.
Amefafanua kuwa kwa Aprili ,2022 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa shilingi 321/Lita sawa na asilimia 21.45 mtawalia.
“Vilevile katika toleo lililopita bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa shilingi 320.33/Lita sawa na asilimia 13.29, Shilingi 288.50/Lita sawa na asilimia 12.69 na shilingi 472.41/Lita sawa na asilimia 22.72 mtawalia,”amefafanua
Maganga amesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini ikihusisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa 2 Machi,2022.
“Kwa mwezi Machi mwaka huu,bandari ya Mtwara imepokea mafuta ya dizeli tu hivyo kwa Aprili 2022 bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli kwa mikoa ya Kusini yaani Lindi na Ruvuma zitakuwa sawa na zile zilizotangazwa tarehe 2 Machi,2022,
Kwa upande wa dizeli kwa mwezi Aprili 2022,Bei za rejareja na jumla za dizeli zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la mwezi uliopita ,bei ya rejareja ya dizeli imeongeza kwa shilingi 281/Lita sawa na asilimia 11.12 na bei ya jumla ya dizeli ikiwa imeongeza kwa shilingi 279.99/lita sawa na asilimia 11.67,”amefafanua.
Ameeleza kuwa kwa kuwa hakuna matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka bandari ya Dar Es Salaam na kwamba bei za rejareja za mafuta hayo katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa Kupitia bandari ya Dar Es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.
“Mabadiliko haya ya rejareja yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika Soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola za marekani,hivyo EWURA inaukumbusha Umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia Kupitia simu za mkononi Kwa kupiga namba *152*00#,”amefafanua
Hata hivyo Maganga amefafanua kuwa Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo zisivuke bei kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa kama ilivyokokotolewa Kwa kutumia formula na kanuni za EWURA zinazopanga Bei za mafuta za mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia gazeti la Serikali namba.57 la tarehe 28Januari mwaka huu.