Na Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amesema umri wa ukomo katika mikopo kwa vijana umeongezwa kutoka miaka 35 hadi 45.
Dkt. Dugange ameyasema hayo leo Februari 7,2025 Bungeni hapa Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Boniphace Gutere aliyehoji ni lini Serikali itatenga dirisha maalum la mikopo ya wanaume waliovuka umri wa vijana na kuendelea.
“Mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 37A ya Mwaka 2018 na Kanuni za Usimamizi na Utoaji wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za Mwaka 2024,”amesema.
Amesema kwa mujibu wa Sheria hii, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba. Makundi haya yana fursa ndogo ya kupata mikopo katika taasisi nyingine za fedha kwa kuwa yanakosa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba.
Aidha, ameongeza kuwa makundi mengine ambayo sio walegwa wa mikopo hiyo wanashauriwa kupata mikopo kupitia taasisi nyingine za fedha, biashara na programu za kijasiriamali zinazohusisha makundi yote.
Pia Dkt. Dugange amewasisitiza Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwamba umri wa vijana umeongezeka kutoka kikomo cha miaka 35 mpaka 45 ili wanufaika waongezeke na kupata fursa hiyo ambayo ipo kwaajili yao.
“Baada ya kukamilika kwa kanuni za mikopo ya 10% za mwaka 2024 miongozo tayari imekwisha kutolewa na kupelekwa katika Halmashauri zote 184 na tangu mikopo imeanza kutolewa vijana wanapewa mikopo wote wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 45,”amesema.