Featured Kitaifa

WAZIRI KIJAJI: HAKUNA UTARATIBU WA KUKAGUA WENYE MKAA MAJUMBANI

Written by mzalendo

Serikali imesema sio sahihi na hakuna utaratibu wa kufanya ukaguzi katika
kila kaya ili kubaini kama zinazotumia kuni au mkaa na badala yake
kinachotakiwa ni kufuatilia na kuhakikisha misitu haikatwi ovyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Kibamba Issa Mtemvu aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu madai ya
kuwatafuta watumiaji wadogo wa mkaa kwenye makazi.

Amesema kuwa ukimfuata mwananchi mmoja mmoja huwezi kujua kama
mkaa huo alionao una kibali au hauna hivyo ametoa wito kwa taasisi za
Serikali kurejea masharti ya matumizi ya kuni na mkaa.

Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa ili kuhakikisha kila mwananchi
anamudu gharama za nishati safi ya kupikia ikiwemo ya gesi, Serikali
inashirikiana na wadau mbalimbali katika kupunguza bei za nishati hiyo na
vifaa vyake.

Halikadhalika, amesema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kufungua milango
kwa wawekezaji wa nishati hiyo kuwekeza katika nishati safi hiyo rafiki kwa
mazingira ili kulinda misitu isiendelee kukatwa.

Katika jibu la msingi la Mbunge Mtemvu, Mhe. Dkt. Kijaji amesema Serikali
imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia (2024-2034) ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika
matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mkakati huu unalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania
wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na kupunguza gharama
za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.

Halikadhalika amesema kuwa Mkakati umelenga kuimarisha upatikanaji wa
malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia; kuhamasisha
uwekezaji katika nishati safi ya kupikia.

Katika kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa
matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na kuni na mkaa, Mhe. Dkt.
Kijaji amesema Serikali inaendelea kuta elimu ili kupunguza ukataji wa miti
Vilevile, amesema kuwa Serikali kupitia Mkakati wa Nishati Safi imeweka
kipengele cha kuona uwezekano wa kushusha bei ya nishati safi ambayo pia
inakwenda sanjari na kuweka ruzuku katika eneo hilo.

Amebainisha hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ilemela Mhe. Dkt.
Angeline Mabula aliyeuliza Serikali haioni uwezekano wa kutoa ruzuku katika
mitungi ya gesi.

About the author

mzalendo