Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO AHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA SEHEMU ZA BIASHARA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akizungumza na wadau wa mazingira mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa mazingira na kupanda miti katika ufukwe wa Feri Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akijumuika na viongozi na wadau wa mazingira kushiriki zoezi la usafi wa mazingira katika ufukwe wa Feri Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo (wa pili kushoto) akiwa meza kuu na viongozi wengine kuanzia kushoto Mkuu wa Wilaya Kigamboni Fatma Nyangasa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa na Balozi wa Mazingira ambaye pia ni kiongozi wa  Winfrida Shonde wakati wa zoezi la usafi wa mazingira na upanda miti katika ufukwe wa Feri Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo na viongozi wengine akipanda mti katika ufukwe wa Feri Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

…………………………………………………

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt Seleman Jafo amehamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara na huduma za kijamii kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira.

Ametoa hamasa hiyo wakati akijumuika na viongozi na wadau mbalimbali wa mazingira kushiriki katika zoezi la kusafisha maeneo ya fukwe eneo la Feri wilayani ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam Machi 26, 2022.

Sambamba na zoezi hilo Dkt. Jafo akizindua kampeni ya ‘Soma na Mti’, alisema Serikali inahimiza maeneo yote wanayokaa watu yakiwemo stendi za mabasi, daladala, masoko, maeneo ya biashara mbalimbali, taasisi za Serikali zote yawe katika hali ya usafi.

Aidha waziri huyo alipongeza uongozi wa Wilaya ya Kigamboni na mkoa kwa ujumla kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuweka maeneo yote katika hali ya usafi na hivyo kupunguza magonjwa ya mlipuko.

Akizungumzia kampeni ya ‘Soma na Mti’ alisema ni muhimu kwa kila mwanafunzi kutoka shule na vyuo kupanda miti ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inayokabili taifa na dunia kwa ujumla.

“Lengo la kampeni ya Soma na Mti ni kupanda miti milioni mia mbili na sabini na sita kwa mwaka, tuna wanafunzi milioni kumi na nne na nusu katika shule za msingi, sekondari, vyuo sasa kila halmashauri imeelekezwa kupanda miti milioni moja na nusu,” alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Hassan Rugwa aliwashukuru wadau wote wa mazingira kwa kutenga muda wao na kushiriki zoezi hilo la usafi.

Pia Rugwa alimpongeza Waziri Jafo kwa kujitoa katika kuhakikisha mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu yanawekwa katika hali ya usafi na kutunzwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa alisema kampeni ya kuiweka wilaya hiyo katika hali ya usafi sambamba na kupanda miti inaendelea.

Alisema kuwa kila mmoja anawajibika katika kuhakikisha inakuwa safi huku akisisitiza kampeni hiyo inaenda sambamba na udhbiti wa utupaji wa taka ovyo.

About the author

mzalendoeditor